1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trier kuadhimisha miaka 200 ya kuzaliwa Karl Marx

Sekione Kitojo
5 Mei 2018

Polisi mjini Trier Ujerumani wanajitayarisha na maandamano ambayo yatawahusisha mamia ya waandamanaji Jumamosi(05.05.2018) wakihudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 200 ya kuzaliwa ,muasisi wa nadharia ya ukomunisti.

https://p.dw.com/p/2xD2p
200. Geburtstag Karl Marx | Grabstätte Marx' auf dem Friedhof von Highgate in London
Picha: imago/Camera4

"Tuna matumaini  kwamba  kila  mmoja  ambaye  atataka kushughulika  na  suala  hili la  Marx atafanya  hivyo  katika  njia  ya utulivu," msemaji  wa  mji  huo Michael Schmitz  alisema. "Iwapo unataka  kumkosoa  Marx , unakaribishwa  kufanya  hivyo, lakini  sio kwa  kutumia  nguvu  na  ghasia  ama hasira  za  uharibifu."

Deutschland Trier 200. Geburtstag von Karl Marx | Jean-Claude Juncker
Jean-Claude Juncker rais wa Halmashauri ya Umoja wa UlayaPicha: Reuters/W. Rattay

Sherehe  ya  ufunguzi Ijumaa  jioni  mjini  Trier ilianza kwa  hotuba iliyotolewa  na  rais  wa  halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Jean-Claude Juncker.

"Unapaswa  kumuelewa  Karl Marx  katika  wakati  wake,"  Juncker alisema, na  kuongeza  kwamba  Marx  hawezi  kuwajibishwa kutokana  na  uhalifu  uliotendwa  na  wafuasi  wake muda mrefu baada  ya  kifo  chake mwaka  1883.

Maonesho  makubwa  matatu yanatarajiwa  kufunguliwa kwa  ajili  ya umma  kuanzia  leo  Jumamosi.

Lakini kilele  cha  sherehe  hizo  za  siku  ya  kuzaliwa kinatarajiwa kuwa  leo  Jumamosi , wakati picha  kubwa ya Marx , iliyotolewa zawadi  na  China , inatarajiwa  kuzinduliwa. Makamu  mkuu  wa chama  cha  waandishi  cha  PEN  nchini  Ujerumani  kimeomba kwamba  uzinduzi ucheleweshwe, hata hivyo, hadi  pale  mshairi kutoka  China  Liu  Xia atakapoachiliwa  kutoka  kizuwizi  cha nyumbani  na  kuondoka  nchini  China.

Deutschland Trier 200. Geburtstag von Karl Marx
Kitabu cha Karl MarxPicha: Reuters/W. Rattay

Wakosoaji  na  waandamanaji  wanatarajiwa  kuonekana  na kueleza  kile  wanachosimamia. Chama  kinachopinga  wahamiaji cha  Alternative for Germany AfD kinapanga  kumbukumbu  ya wahanga  wa  ukomunisti kwa  maandamano  ya  kimya  kimya, na ukeshaji sehemu  kadhaa  kwa  ajili  ya  kupigwa  marufuku  kwa vuguvugu  la  kidini  nchini  China  la  Falun Gong pia  yanapangwa kufanyika.

Maandamano  ya  waungaji mkono nadharia za Marx

Wakati  huo  huo , muungano  wa  waungaji  mkono  nadharia  ya Marx , ikiwa  ni  pamoja  na  wanachama  wa  chama  cha  Die Linke , chama  cha  mrengo  wa  kushoto  nchini  Ujerumani  pamoja  na chama  cha  Kikomunist nchini  Ujerumani,  pia  vimepanga  kufanya maandamano "dhidi  ya  ubepari  na  unyonyaji."

Deutschland Trier 200. Geburtstag von Karl Marx | Karl-Marx-Statue, eingehüllt
Picha ya kuchonga ya Karl Marx itakayozinduliwa ikiwa ni zawadi kutoka ChinaPicha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Kwa  mujibu  wa  polisi  maandamano  ya upande  mwingine  dhidi ya  yale  ya  chama  cha  AfD pia  yanapangwa  kufanyika. Polisi watakuwapo  pamoja  na  maafisa  kadhaa  wa  mjini  Trier. "Idadi kubwa  ya  mikutano  na  matukio  yanaleta  changamoto  ya  aina yake," mkuu  wa  polisi Ralf  Kraemer  amesema.

200. Geburtstag Karl Marx | Konterfeis von Marx, Engels und Lenin
Karl Marx atimiza miaka 200 tangu kuzaliwa, picha inamuonesha Karl Marx(kushoto) Friedrich Engels na Vladimir LeninPicha: imago/UIG

Katikati  ya  mji  wa  Trier , katika  jimbo  la  Rhineland-Palatinate kumewekwa  maandishi  maalum  "Karl Marx (1818-1883), Maisha - Kazi - Ushawishi  hadi  sasa"  - ambako  zaidi  ya  maonesho 400 kutoka  karibu  dazeni  moja  ya  majimbo  nchini  Ujerumani  katika makumbusho  mbili  za  mjini  Trier yatafanyika.

Pia  kuna  maonesho  mawili  ya  washirika  katika  makumbusho  ya mji  huo  ya  Kanisa na  katika  nyumba  ya  Karl Marx , sehemu alipozaliwa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo /  dpae

Mhariri: Caro Robi