Tanzania, Kenya na Uganda zatinga fainali za Afcon | Michezo | DW | 24.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Tanzania, Kenya na Uganda zatinga fainali za Afcon

Timu ya taifa ya Tanzania imejiunga na timu nyingine kutoka Afrika mashariki, Kenya na Uganda kukamilisha historia kwa mara ya kwanza  timu hizo kushiriki katika  fainali  za kombe la mataifa ya Afrika ,Afcon.

Timu  ya  taifa  ya  Tanzania ilifanikiwa  kupata  mabao 3-0 dhidi  ya  majirani  zao  wa Uganda  katika  mchezo  ambao ulikuwa  ni  lazima  Taifa  Stars kushinda. Uganda imeshika nafasi  ya  kwanza  katika  kundi L, ambalo  lilikuwa  na  timu  za  Uganda, Cape Verde, Lesotho  na  Tanzania. Kwa  ushindi  huo  Tanzania  inashika  nafasi  ya  pili  baada  ya Uganda , baada  ya  mchezo  kati  ya  Lesotho  na  Cape Verde  kutoka  sare  bila  ya kufungana.

Afrika Fußball AFCON Games (DW/ T.Khumalo)

Mashabiki wa kandanda wakishangiria katika michuano ya Afcon

Tanzania  imetimiza  pointi 8 , ikifuatiwa  na  Lesotho  ambayo  baada  ya  sare  dhidi  ya cape Verde itakuwa  na  pointi 6 tu.

Ni  mara  ya  kwanza  kwa  Tanzania , Uganda  na  Kenya  kutinga  kwa  pamoja  katika fainali  hizo za  kombe  la  mataifa  ya  Afrika  tangu  kuanzishwa kwake.

Tanzania  imewahi  kushiriki  katika  fainali  hizo  miaka  38  iliyopita, lakini Uganda  imewahi kushiriki  mara  mbili.

Kenya  ilicheza  na  Ghana  siku  ya  Jumamosi  kutafuta  nafasi ya  kwanza  ama  ya  pili katika  kundi  lake la  F , ambapo  mchezo  wake mjini  Nairobi ulimalizika kwa  Ghana kujipatia  ushindi  wa  bao 1-0.

Afrika Fußball AFCON Games (DW/ T.Khumalo)

Mashabiki wa kandanda wakishangiria ushindi katika michuano ya Afcon

Katika  michezo  ya  leo timu ambazo  zimefanikiwa  kuingia  katika  fainali  hizo  za  Afcon 2019  ni  pamoja  na DRCongo  ambayo  iliishinda  Liberia  kwa  bao 1-0, na  kuungana  na Zimbabwe  kufuzu  kucheza  katika  fainali  hizo. Zimbabwe  iliishinda Congo Brazzaville  kwa mabao 2-0.

Timu  nyingine  iliyofuzu ni Benin  iliyoifunga  Togo  mabao 2-1  nyumbani. Togo inajiunga pamoja  na  Algeria  katika  fainali  hizo. Afrika  kusini na  Libya zinapambana , ambapo Libya  inalazimika  kushinda, wakati  Afrika  kusini  inahitaji  sare  kuweza  kufuzu.