1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha ya 61 ya kimataifa ya filamu-Berlinale

10 Februari 2011

Filamu iliotengenezwa upya ya cowboy miaka ya sitini kuhusu msichana alieazimia kulipiza kisasi cha baba yake inafunguwa Tamasha la Filamu la Berlin (Berlinale) leo hii.

https://p.dw.com/p/10FFu
Nembo ya Berlinale 2011Picha: Internationale Filmfestspiele Berlin

Filamu ya True Grit iliyotayarishwa na Joel na Ethan Coen waongozaji filamu wa Marekani washindi waliopendekezwa kwa tuzo ya Oscar pia itaanzisha Berlin michuano ya kuanza kuwania Academy Awards yaani tuzo hizo za Oscar za Marekani ambazo zitatangazwa mjini Los Angeles Marekani baadae mwezi huu.

Filamu hiyo True Grit ambayo waigizaji wake ni Jeff Bridges, Matt Damon na Josh Brolin imeteuliwa kupokea tuzo 10 za Oscar.

Mara ya mwisho waongozaji hao wa filamu ambao ni ndugu walikuwako Berlin kwa tamasha hilo la filamu miaka 13 iliopita kwa ajili ya filamu ya Big Lebowski.

Deutschland Berlin Kultur Film Berlinale 2011 Jury Gruppenbild
Jopo la wasimamiziPicha: dapd

Sambamba na waigizaji hao maarufu kutoka filamu ya True Grit mwanamuziki mashuhuri Madonna,muigazaji sinema wa kike wa Uingereza Vanessa Redgrave,muigizaji mashuhuri wa kiume wa Marekani Kevin Spacey na muigizaji sinema wa kike wa Marekani alieteuliwa kwa tuzo ya Oscar Gabourey Sidibe wanatarajiwa kuwepo katika tamasha hilo mjini Berln.

Muigizaji sinema wa kiume wa Uingereza Colin Firth pia atakuwepo mjini Berlin kwa ajili ya tamasha hilo.Muigazaji huyo ameteuliwa kwa tuzo ya Oscar kutokana na kuwa muigizaji bora wa kiume ambapo aliigiza kuwa Mfalme George wa Sita katika filamu inayoitwa King's Speech.

King Speech iliyotayarishwa na muigizaji filamu wa Uingereza Tom Hooper imeteuliwa kupokea tuzo 12 za Oscar.Filamu zote mbili King Speech na True Grit hazikujumuishwa katika mchuano mkuu wa tamasha la Berlinale.

Filamu kadhaa zinazoonyeshwa Berlin huko nyuma zimekuwa zikiingia katika kundi la michezo ya sinema inayoteuliwa kushinda tuzo za Oscar.

Hata hivyo kwa kiasi kikubwa michezo au filamu zinazoingizwa katika mchuano mkuu wa Berlinale inahusu wasi wasi wa hali ya kisiasa na mada za malumbano katika jamii.

Flash-Galerie Film Das Leben danach Matt Damon
Matt Damon-muigizaji wa filamu True GritPicha: Warner Bros.

Kwa ajili hiyo zinakuwa haziko katika nafasi kubwa sana ya kujipatia tuzo za Oscar.

Miongoni mwa filamu zitakazoonyeshwa katika tamasha hili la Berlinale ni Torinoi Lo ya muigizaji filamu wa Hungary Bel Tarr,filamu kuhusu mwanafalsafa wa Ujerumani na The Forgiveness of Blood ya Joshua Martson kuhusu familia mbili za Albania zilozijizonga kwenye visasi.

Katika mwaka wake wa 61 tamasha hilo mjini Berlin litakagua takriban filamu 400 kutoka nchi 58 duniani.

Berlinale pia linakabiliwa na ushindani unaozidi kukua kutokana na kuchipuka kwa matamsha mapya ya filamu hivi karibuni mjini Rome,Abu Dhabi, Doha, Dubai na Marrakesh wakati matamasha ya filamu ya Toronto na Sundance yakizidi kupata hadhi ya kimataifa.

Likiongozwa na muigizaji sinema wa kike wa Ufaransa Isabella Rossellini jopo la watu saba inabidi lichaguwe filamu 16 kwa ajili ya tuzo za juu za Berlinale filamu bora zitakazopokea tuzo za 'Dubu wa Dhahabu'.

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa

Mpitiaji:Abdul-Rahman