Sudan yahimizwa kukomesha mashambulizi ya Darfur | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sudan yahimizwa kukomesha mashambulizi ya Darfur

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito kwa Sudan kusitisha mashambulio ya angani ya majuma matatu ambayo yamesababisha maafa katika jimbo la mgogoro la Darfur.

Wakimbizi katika kambi ya Abou Shouk kaskazini mwa Darfur

Wakimbizi katika kambi ya Abou Shouk kaskazini mwa Darfur

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake mjini New York imesema,Ban Ki-Moon ameihimiza serikali ya Sudan kusitisha mashambulio yote katika jimbo la Darfur,iheshimu kikamilifu makubaliano ya amani ya Darfur,maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.Wakati huo huo ametoa wito kwa serikali na makundi yote kusitisha mapigano na vile vile pande zote zishirikiane kwa ukamilifu na wajumbe wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanaojaribu kuleta maafikiano ya kukomesha mgogoro unaoteketeza jimbo la Darfur. Kuambatana na Ban,ripoti zimesema kuwa mashambulio ya bomu yaliyofanywa kaskazini ya Darfur yamesababisha wakazi zaidi kukimbia makwao.Akaongezea kuwa katika kijiji cha Um Rai shule moja ilishambuliwa kwa makombora yaliyorushwa kutoka helikopta ya serikali.

Lakini balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Abdel-Mahmood Abdel-Haleem amesema,yeye alikwenda kuonana na Katibu Mkuu Ban kukanusha ripoti za mashambulio hayo.Baadae alipozungumza na waandishi wa habari,mwanadiplomasia huyo wa Sudan alisema,ripoti hizo ni uwongo uliosambazwa na wale wanaotaka kufuja majadiliano ya amani.

Kwa upande mwingine nchini Marekani siku ya Jumatano,zaidi ya wabunge 100 waliwasilisha barua kwa Rais Hu Jintao wa China.Katika barua hiyo wabunge hao wameonya juu ya kile kilichoitwa “maafa” kwa michezo ya Olimpik ya mwaka 2008, pindi Beijing haitojitahidi zaidi kuzuia umwagaji wa damu katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Mbunge wa California Tom Lantos wa chama cha Demokratik,ambae pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi kuhusika na masuala ya kigeni,aliungwa mkono na wabunge 106 katika barua hiyo kali.Mbunge Lantos alienusurika Maangamizi Makuu,ni mkosoaji mkali wa serikali za kiimla. Katika barua yake,Lantos ameihimiza China ijiepushe kuchafua sifa yake kwa kushirikiana na serikali inayoua kiholela.Amesema,isijichafulie sifa kwa sababu ya faida za kiuchumi.Kibiashara, China ni mshirika mkuu pekee wa Sudan na hunufaika zaidi kutokana na mauzo ya mafuta ya Sudan na kandarasi za ujenzi.Uhusiano wa karibu wa kiuchumi na kisiasa kati ya Sudan na China,uliifanya Beijing kuwa na dhima ya kupinga maazimio ya Umoja wa Mataifa yaliyopendekeza kupeleka walinzi wa amani katika jimbo la Darfur.

Kwa sababu ya uhusiano huo wa karibu,mbunge Lantos katika barua yake ameihimiza China kuishinikiza serikali ya Sudan kuchukua hatua za kukomesha mashambulio ya kijeshi katika jimbo zima la Darfur.Vile vile vikosi vya serikali viondoshwe kutoka eneo hilo na Khartoum itoe idhini ya kupelekwa vikosi zaidi vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kulinda amani huko Darfur.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com