Siku ya maji duniani yaadhimishwa kesho | Masuala ya Jamii | DW | 21.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Siku ya maji duniani yaadhimishwa kesho

Ban Ki Moon aonya upungufu wa maji huenda ukaongeza migogoro katika siku za usoni

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Maadhimisho ya kimataifa ya siku ya maji duniani yatafanyika hapo kesho, huku Afrika Kusini ikikabiliwa na mzozo wa kitaifa wa maji. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba upungufu wa maji huenda ukazusha migogoro zaidi katika siku za usoni.

Maadhimisho ya siku ya maji duniani ni wazo lililoanza katika mkutano wa shirika la mazingira na maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCED, uliofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil mnamo mwaka wa 1992. Baraza kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio lililoitaja tarehe 22 mwezi Machi kuwa siku ya maji duniani.

Siku hiyo ilianza kuadhimishwa mnamo mwaka wa 1993 kulingana na mapendekezo ya shirika la mazingira na maendeleo la Umoja wa Mataifa katika ibara ya 18 ya ajenda 21 ya shirika hilo inayozungumzia raslimali ya maji.

Nchi mbalimbali zimeombwa ziitumie siku ya maji duniani kutekeleza mapendekezo ya Umoja wa Mataifa na kuunda mikakati madhubuti kuhakikisha ugavi na usimamizi bora wa maji katika ngazi ya kitaifa.

Afrika Kusini yakabiliwa na mzozo wa maji

Afrika Kusini imekuwa ikiadhimisha wiki ya maji tangu Jumatatu wiki hii kabla maadhimisho ya siku ya maji duniani hapo kesho. Maadhimisho haya lakini yanafanyika wakati kukiwa na mzozo wa kitaifa kuhusu uwezo wa serikali kuwapa wananchi maji safi ya kunywa.

Kufikia mwanzoni mwa mwezi uliopita mzozo huo ulikuwa haujumilishi sekta yote ya maji nchini Afrika Kusini. Kulikuwa na matatizo ya maji ya hapa na pale na watu wengi waliingiwa na wasiwasi kuhusu kuzorota kwa huduma za maji na usafi, lakini watu wachache walilieleza tatizo hilo kuwa la kitaifa.

Hata hivyo viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini, cha Democratic Alliance, na maafisa wa shirika la kitaifa linalopigania kuwalinda watu kutokana na athari zinazohusiana na nyuklia, NNR, kwa pamoja walitoa ripoti za kuishutumu idara inayosimamia maswala ya maji na misitu nchini Afrika Kusini, DWAF, kwa kushindwa kutoa huduma nzuri.

Ripoti ya shirika la NNR iliijulisha serikali kuhusu maji taka kutoka shughuli za uchimbaji madini kuingia katika mfumo wa maji wa ardhini. Aidha ripoti hiyo ilisema mboga na samaki wanaovuliwa katika maeneo ya maji karibu na mji mkuu Johannesburg, wameathirika kutokana na madini ya uranium.

Ripoti ya chama cha Democratic Alliance, iliyopewa jina onyo la tufani, mzozo mkubwa wa maji unakaribia, ilisema mchanganyiko wa uchafuzi wa vyanzo vya maji na usimamizi mbaya wa mabwawa, mifereji ya maji taka na viwanda vya kuyatia dawa maji hayo, yamesababisha kuwepo kitisho kikubwa kwa ugavi wa maji nchini Afrika Kusini. Kampeni kubwa ya kuwahamasisha raia kuhusu wiki ya maji imekuwa ikiendelea nchini humo huku maafisa wa idara ya maji wakisambaza vipeperushi vya maelezo katika vituo vya mafuta mabarabarani nje ya mji wa Johannesburg na katika barabara kuu kuelekea eneo la mashariki la nchi hiyo.

Ban Ki Moon aonya kuhusu upungufu wa maji

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameonya kwamba uupungufu wa maji huenda ukazusha migogoro zaidi katika siku za usoni. Akiwahutubia wafanyabiashara matajiri, wasomi na viongozi wa serikali mbalimbali katika mkutano uliofanyika hivi majuzi mjini Geneva nchini Uswisi, Ban Ki Moon alisema mabadiliko ya hali ya hewa na kuongezeka kwa idadi ya wakaazi duniani kutaifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Anders Berntell, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya kimataifa ya maji mjini Stockholm Sweden, anasema ukosefu wa maji safi ya kunywa kwa watu zaidi ya bilioni moja duniani na ukosefu wa usafi kwa wakaazi zaidi ya bilioni 2.5 ni janga kubwa la kibinadamu lenye maangamizi makubwa.

Kiongozi huyo amesema hali hii inaweza kurekebishwa kwa kuboresha utawala na usimamizi wa maji, kuongeza ufadhili na kuendeleza juhudi za kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa, likiwemo lengo la kuangamiza umaskini uliokithiri, baa la njaa na kuhakikisha kuna usafi na maji ya kutosha.

 • Tarehe 21.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DSRe
 • Tarehe 21.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DSRe
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com