Siasa ya nje ya Ujerumani itakua ya aina gani? | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.10.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Siasa ya nje ya Ujerumani itakua ya aina gani?

Waziri mpya wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle anasema siasa ya nje haitabadilika sana

Waziri mteule wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle

Waziri mteule wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle

Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anaitwa Guido Westerwelle. Yeye ni kiongozi wa chama cha Free Democrats FDP, mshirika mdogo katika serikali mpya ya Angela Merkel. Chama hicho cha kiliberali kilikuwa upande wa upinzani miaka kumi na moja iliyopita.

Kimsingi miongozo ya sera za nje na usalama itabakia kama ilivyo. Lakini kuna mambo kadhaa mapya yanayotiliwa mkazo katika mkataba wa muungano wa serikali mpya ya Ujerumani kama alivyoeleza Guido Westerwelle.

" Katika sera za nje haimaanishi tu kuendelea kama hapo awali bali ni kuwa na mwanzo mpya vile vile."

Kuambatana na mkataba wa muungano, sera za nje kwa sehemu kubwa zitafuata mwongozo ule ule. Na nguzo ya sera hizo imebakia imara:Kwa Ujerumani, Umoja wa Ulaya na NATO ni washirika walio muhimu kabisa; ni lazima kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na Marekani sawa na ushirikiano mzuri pamoja na Urusi.Mkataba wa muungano unasisitiza uhusiano maalum wa Ujerumani kuhusu Israel na kueleza kuwa serikali mpya itapigia debe suluhisho la mataifa mawili.

Majadiliano ya kuomba uanachama wa Umoja wa Ulaya yafuatilize matokeo yalio wazi, yaani kuhusu Uturuki, hakuna uanachama wa moja kwa moja. Majadiliano pamoja na China kuhusu utawala wa kisheria yaimarishwe na mazungumzo pamoja na Iran kuhusu mradi wake wa nyuklia yaendelee kufanywa. Ikihitajika,Ujerumani itaunga mkono kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi.

Kwa kweli, kusitarajiwe kipya cha kushangaza hasa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa nguzo ya sera za nje katika serikali mpya. Hata hivyo Guido Westerwelle atataka kuweka muhuri wake pia. Yeye anataka kufuata nyayo za Hans-Dietrich Genscher aliekuwa maarufu sana kama waziri wa nje wa chama cha kiliberali. Katika mkataba wa kuunda serikali mpya ya muungano, FDP hasa kimeingiza vipengele vipya katika sera za usalama

Der FDP-Vorsitzende Guido Westerwelle, links, und der frühere Aussenminister Hans-Dietrich Genscher

Westerwelle na mwanasiasa aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani,Hans- Dietrich Genscher

„Tunachotaka ni kuondosha silaha za mwisho za atomu zilizowekwa Ujerumani.- kwa hivyo suala hilo litajadiliwa pamoja na washirika wetu.“

Hapo kinachomaanishwa ni mabomu ya atomu yaliyowekwa na Marekani nchini Ujerumani kama sehemu ya silaha za NATO. Katika suala hilo Westerwelle atapokewa vizuri na Barack Obama kwani rais huyo wa Marekani binafsi anaunga mkono kupunguza silaha za nyuklia duniani.

Na kuhusu Afghanistan ni machache yaliyo mapya. Mkataba wa muungano haukugusia suala la kuyarejesha nyumbani majeshi ya Ujerumani. Na katika suala la uandikishaji wa lazima jeshini kumepatikana maafikiano. FDP kimetaka kuondosha sheria hiyo kinyume na CDU kinachotaka kuendelea kuwalazimisha vijana wa kiume kuhudumia jeshini kwa muda fulani. Sasa washirika wapya wamekubaliana kuwa kuanzia mwaka 2011 kipindi hicho kitafupishwa kuwa miezi 6 badala ya miezi 9. Wataalamu wana shaka iwapo miezi sita inatosha kutoa mafunzo timamu ya kijeshi.

Mwandishi: N.Werkhäuser/ZPR/P.Martin

Mhariri: M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.10.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KGAR
 • Tarehe 27.10.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KGAR
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com