Sera ya kutetea viwanda nchini ni mtindo hatari | Magazetini | DW | 16.02.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Sera ya kutetea viwanda nchini ni mtindo hatari

Madai ya ngongeza ya mishahara katika sekta ya huduma za jamii, sera ya kutetea viwanda vya nchini,malipo ya marupurupu kwa wakuu wa benki ni miongoni mwa mada zilizoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu.

Basi tukianza na gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linasema:

Sera ya kulinda viwanda vya nchini husababisha madhara makubwa kuliko hiyo faida inayopatikana.Kwani hatua zinapochukuliwa kujikinga dhidi ya wengine,hatimae kila nchi itabakia na bidhaa zake.Kinachotisha ni kuwa si Urusi,Ufaransa au Marekani inayotaka kusikiliza ukweli huo.Kwani hali ya kiuchumi ikizidi kuwa mbaya,wanasiasa wapo tayari kuchukua kila aina ya hatua.Inaeleweka lakini huo ni mtindo hatari kwani hatimae biashara duniani itakuja kwama na viwanda vitafilisika.

Gazeti la NORDKURIER limegusia mada iliyohamakisha umma na serikali nchini Ujerumani.Marupurupu yanayolipwa kwa wakuu wa benki zilizoomba msaada wa serikali kupambana na mzozo wa fedha.Likiendelea linaandika:

Badala ya kupunguziwa malipo ndio kwanza wanapewa marupurupu kwa hasara walizosababisha-hilo ni jambo lisiloeleweka hata kidogo.Hata ikiwa ahadi za marupurupu zilitolewa kabla ya uchumi kuporomoka duniani, malipo hayo ni sehemu ya mambo yaliyosababisha mzozo wa uchumi.

Gazeti la TRIERISCHER VOLKSFREUNDE likiendelea na mada hiyo hiyo linashauri hivi:

Labda ingefaa kuitupia jicho Marekani.Kwani huko msaada wa Rais Barack Obama kufufua uchumi,unafungamanishwa na masharti.Kimsingi,benki zilizopata msaada wa serikali zinaruhusiwa kutoa marupurupu baada tu ya kuilipa serikali fedha zilizopokewa kama msaada.Huo unaweza kuwa mfano kwa Ujerumani pia na ikihitajika,hiyo iwe sheria.

Tukibadilisha mada, tunatazama uhariri wa gazeti la DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN likistaajabu na kusema:

Baadhi kubwa ya wafanyakazi wakihofia nafasi zao za ajira katika kipindi hiki kigumu chenye matatizo ya kiuchumi,sekta ya huduma za jamii inathubutu kudai nyongeza ya mishahara.Wafanyakazi katika sekta hiyo wanataka kuwa na uhakika fulani kuhusu nafasi zao za kazi na vile vile kuongezewa mishahara kwa hadi asilimia saba.Kwa hivyo si ajabu kuona kuwa ni wachache wanaoelewa madai kama hayo.Ni dhahiri kuwa itakuwa vigumu mno kwa pande zote mbili zinazohusika na mzozo wa nyongeza ya mishahara,kumaliza mgogoro huo haraka.Kusiwepo tena mvutano wa majuma 15 kati ya waajiri na waajiriwa kama ilivyokuwa wakati wa majadiliano ya safari ya mwisho.Pande zote mbili zinawajibika kuzuia mvutano mrefu lamalizia DRESDNER NEUSTE NAHRICHTEN.