Senegal washinda AFCON dhidi ya Morocco
19 Januari 2026
Uwanja wa Mwanamfalme Moulay Abdellah mjini Rabat ulizizima wakati wa mechi ya mshikemshike kati ya Simba wa Teranga Senegal na wenyeji Morocco wanaofahamika pia kama Simba wa Atlas. Dakika 90 za mwanzo zilimalizika bila ya simba hao kufungana.
Baada ya dakika nane tu katika muda wa nyongeza, Morocco walipata penati iliyozua vurugu baada ya Kocha wa Senegal Pape Thiaw kuwataka wachezaji wake kuondoka uwanjani na kususia mechi kama ishara ya kupinga uamuzi huo. Ilikuwa hali ya sintofahamu lakini mchezaji Sadio Mané aliwataka wachezaji wenzake kurejea uwanjani na "kupambana kiume". Hasira ya wachezaji wa Senegal ilitokana pia na bao lao kukataliwa kabla ya penati hiyo.
Baada ya vurumai, mchezo uliendelea na katika hali ya kushangaza mchezaji wa Morocco Brahim Diaz aliipiga penati iliyodakwa kirahisi mno na golikipa wa Senegal Edouard Mendy. Mashabiki wa Senegal walishangilia kwa kishindo huku Morocco wakipigwa na butwaa. Sasa, ni kama mechi ilianza upya kwa ari na kasi ya ajabu huku kila timu ikijaribu kuonyesha ubabe wake.
Bao la ushindi na ukosoaji wa Morocco
Dakika nne baada tu ya penati iliyozua utata, Pape Gueye alipachika bao maridadi kabisa ambalo golikipa wa Morocco Yassine Bounou hakuwa na uwezo wowote wa kulizuia. Wachezaji na mashabiki wa Senegal walishangilia kwa hisia, huku bao hilo la Gueye likichukuliwa kama lilokuja kuwafuta machozi na kuwapa matumaini zaidi huku Sadio Mané akipongezwa pia kwa uamuzi wake wa kuwataka wachezaji kurejea uwanjani.
Kocha wa Morocco Walid Regragui alimtetea mchezaji wake na kukosoa uamuzi wa mwenzake wa Senegal akisema kulikuwa na muda mwingi kabla hajapiga penalti na hilo bila shaka lilimvuruga.
" Mechi hii imetoa picha mbaya kuhusu Afrika na ni ya aibu. Kocha anapowaambia wachezaji wake waondoke uwanjani. Lazima uwe na busara unaposhinda na kushindwa. Alichofanya Pape Thiaw ni aibu kwa Afrika," alisema Kocha huyo wa Morocco.
Mashambulizi ya lala salama, ukosoaji wa FIFA
Hata hivyo Morocco walizidisha mashambulizi ya hapa na pale bila mafanikio huku wakiponea kufungwa bao la pili pia katika dakika za lala salama. Kipenga cha mwisho kilipigwa na hatimaye Senegal wakaibuka washindi mara mbili wa michuano hiyo ya Afcon baada ya mwaka 2021 na kukata matumaini ya Morocco ambao mara ya mwisho kushinda kombe hilo ilikuwa mwaka 1976.
Kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa, Rais wa FIFA Gianni Infantino amekosoa vikali mienendo ya "baadhi ya wachezaji wa Senegal" akisema ni "matukio yasiyokubalika" ambayo yameweka kiwingu kwenye ushindi wao katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025 , akisisitiza kuwa haikubaliki kuondoka uwanjani kwa namna ile. Hata hivyo timu ya Morocco ililalamikiwa mno kwa kupendelewa na waamuzi wa michezo, malalamiko yaliyoshuhudiwa katika mechi kadhaa ikiwa ni pamoja na ile dhidi ya Tanzania.