Rufaa ya Bemba yakataliwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rufaa ya Bemba yakataliwa

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-ICC imeamua Jean-Pierre Bemba aendelee kukaa mahabusu.

Rais wa Kongo Joseph Kabila (Kulia) na Jean-Pierre Bemba wakipiga kura katika uchaguzi, 30.07.2006, Kinshasa, Kongo.

Rais wa Kongo Joseph Kabila (Kulia) na Jean-Pierre Bemba wakipiga kura katika uchaguzi, 30.07.2006, Kinshasa, Kongo.

Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jean-Pierre Bemba ataendelea kubakia mahabusu huku akisubiri kesi dhidi yake ya mashitaka ya kuhusika na uhalifu wa kivita, iliyopangwa kufanyika mwaka ujao. Uamuzi huo umefikiwa leo na Mahakama ya Rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-ICC ya The Hague, Uholanzi. Rufaa ya Bwana Bemba iliwasilishwa mwezi Agosti, mwaka huu katika mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-ICC, kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo wa kumuachia mtuhumiwa huyo kwa dhamana. Kesi ya Bemba ambaye anashitakiwa kwa makosa ya kuhusika na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati imepangwa kusikilizwa tena Aprili, mwaka ujao wa 2010 kutokana na kutofikiwa kwa uamuzi wa nchi gani mtuhumiwa huyo atapelekwa wakati akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake hiyo.

Tangu wakati hio Bemba amekuwa akishikiliwa katika mahabusu mjini The Hague huku ikitafutwa nchi ambayo itakuwa tayari kumuhifadhi hadi wakati huo. Jaji Akua Kuenyehia alisema jopo la majaji wa rufaa wameamua kwamba uamuzi uliofanywa na mahakama ya mwanzo uangaliwe upya. Majaji hao waliamua kuwa Bwana Bemba ambaye anaweza akahukumiwa kifungo cha maisha jela endapo atapatikana na hatia, aendelee kukaa mahabusu ili wahanga wa vita hivyo na mashahidi wa kesi hiyo wawe na uhakika kuwa kesi hiyo itasikilizwa katika muda uliopangwa na kwamba watakuwa salama.

Kauli ya Mwanasheria wa Bemba

Mwanasheria wa Bemba, Aime Kilolo anasema, ''Uamuzi uliopitishwa leo na Mahakama ya Rufaa haumalizi suali la kuachiwa huru seneta Jean-Pierre Bemba. Kwa kweli Mahakama ya Rufaa imekosoa jinsi uamuzi wa mahakama ya awali ulivyopitishwa.'' Bemba, mwenye umri wa miaka 47 anashitakiwa kwa makosa matatu ya uhalifu wa kivita na mawili ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu ambayo aliyafanya katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia Oktoba, mwaka 2002 hadi Machi, mwaka 2003. Mashitaka hayo ni pamoja na mauaji, ubakaji na uporaji yanayodaiwa kufanywa na wafuasi wa kundi la Congolese Liberation Movement-MLC, huku wakiyasaidia majeshi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Ange-Felix Patasse katika kukabiliana na jaribio la mapinduzi.

Kesi ya Bwana Bemba itakuwa ni kesi ya tatu kusikilizwa tangu kuanzishwa kwa mahaka hiyo ya ICC iliyopo The Hague, Julai, mwaka 2002. Bemba aliyeondoka nchini Kongo mwaka 2007 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais nchini humo, alikamatwa mjini Brussels, Ubelgiji mwaka 2008, kufuatia waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na ICC. Bemba amekanusha mashitaka yanayomkabili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 02.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kp88
 • Tarehe 02.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kp88
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com