Rouhani asema waliodungua ndege kuadhibiwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rouhani asema waliodungua ndege kuadhibiwa

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema watu wote wanaohusika na kuidungua bila ya kukusudia ndege ya Ukraine wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na ajali hiyo itachunguzwa kwa umakini mkubwa.

Hotuba ya Rais Rouhani iliyorushwa kupitia televisheni imekuwa ya hivi karibuni kabisa katika mlolongo wa matamshi ya kuomba radhi kutoka kwa uongozi wa taifa hilo ambao ni mara chache mno kukubali makosa.

Rouhani amesema "Kwa kuwa vikosi vyetu vimekiri makosa yao waziwazi na kuomba radhi kwa makosa yao. Ilikuwa hatua ya mwanzo na nzuri lakini hatua zinazofuata pia zitachukuliwa."

Rais Rouhani pia ameagiza kuundwa kwa mahakama maalumu ya kushughulikia suala hilo itakayohusisha majaji na wataalamu wengi akisema kesi hiyo si ya kawaida na itakuwa ikifuatiliwa kote ulimwenguni.

Mahakama nchini humo imesema hii leo kwamba baadhi ya watu wanaohusika na ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 176 wamekwishakamatwa. Tangazo hilo linatolewa katika wakati ambapo taifa hilo limegubikwa na maandamano ya raia waliaochukizwa na hatua ya serikali yao awali kukana madai ya kuiangusha ndege hiyo na baada ya siku tatu kukubali kwamba kikosi cha kimapinduzi cha Iran kiliiangusha ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya.

Iran Teheran 2014 | Revolutionsgarde Parade (picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh)

Kikosi cha kimapinduzi cha Iran

Msemaji wa mahakama Gholamhossein Esmaili amesema kumefanyika uchunguzi wa kina na baadhi ya watu wamekamatwa. Taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya mahakama hata hivyo haikueleza ni watu wangapi wanashikiliwa ama majina yao.

Iran yamuita balozi wa Uingereza nchini humo "kipengele kisichofaa".

Wakati Rouhani akiyanyooshea kidole makosa hayo pamoja na uzembe lakini kwa mara nyingine amerudia msimamo wa serikali yake kwamba hatua hiyo ilichochewa na uchokozi wa Marekani na kuongeza kuwa serikali ya Iran kukiri kuiangusha ndege hiyo ni hatua njema ya awali.

Ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Iran kuelekea Kyiv, Ukraine ilikuwa na abiria 167 wa mataifa mbalimba na wafanyakazi wa ndege 9.

Iran Rob Macaire, Britischer Botschafter in Teheran (gov.uk)

Balozi wa Uingereza nchini Iran, Rob Macaire, akliyeshikiliwa kwa muda kufuatia kuhudhuria maandamano haramu

Aidha mahakama nchini humo imesema hii leo kwamba watu 30 wamekamatwa kwenye maandamano na baadhi yao tayari wameachiwa ingawa haikutoa maelezo zaidi.

Katika hatua nyingine mahakama imemtaja balozi wa Uingereza nchini humo Rob Macaire kama "kipengele kisichofaa" hii ikiwa ni kulingana na vyombo va habari vya Iran baada ya maafisa wa Iran kumtuhumu kwa kuhudhuria maandamano haramu licha ya balozi huyo kukana madai hayo.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran iliyomuita balozi huyo ndiyo itakayohusiaka na kutangaza kumtimua balozi huyo aliyekuwa nchini humo tangu 2018.

Msemaji wa mahakama na kiongozi wa dini anayetambulika kwa misimamo mikali, amesema hatua hiyo ndio inamfaa zaidi lakini vinginevyo wafuasi watiifu kwa Jenerali Qassemi Soleimani aliyeuawa kwenye shambulizi la Marekani wangeweza kumuua kwa kumkata vipandevipande.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com