1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya ukweli na maridhiano Liberia yamkuta na hatia rais Sirleaf na vigogo wengine kadhaa

7 Julai 2009

Yapendekeza wasishike nyadhifa za utumishi wa umma kwa miaka 30.

https://p.dw.com/p/Iime
Rais wa Liberia Ellen Johnson SirleafPicha: picture-alliance/dpa

Ripoti mpya iliotolewa na tume ya ukweli na maridhiano nchini Liberia, imependekeza kwamba rais Ellen Johnson Sirleaf na watu wengine kadhaa maarufu wapigwe marufuku kushika nyadhifa zozote za utumishi wa umma kwa muda wa miaka 30. Kiongozi huyo , mwanamke wa kwanza barani afrika kuchaguliwa kidemokrasi kuwa mkuu wa taifa , pamoja na watu wengine 50 wanatajwa kuwa miongoni mwa watu walio gharimia kifedha au kutoa uungaji mkono fulani kisiasa na uongozi kwa makundi ya wapiganaji waliokua na silaha.

Mapendekezo ya tume hiyo ya ukweli na maridhiano yatakabidhiwa kwa bunge la Liberia huenda hii leo ili yachunguzwe . Kwa mujibu wa spika wa bunge hilo Alex Tyler ikiwa baraza la wawakilishi litayaidhinisha mapendekezo hayo na hivyo kuwa sheria kabla ya uchaguzi wa rais 2011, itamaanisha kuwa Bibi Sirleaf hatoweza kugombea tena kwa mhula wa pili.

Orodha hiyo inasemekana kuna jina la Bibi Sirleaf ambaye alichaguliwa rais 2005 na kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasi kuwa mkuu wa taifa, pamoja na watu wengine kadhaa wenye nyadhifa mbali mbali katika serikali yake,akiwemo waziri wa uchukuzi Jackson Doe, kaka yake rais wa zamani Samuel Doe.

Alipoitwa kujieleza mbele ya tume hiyo mwezi Februari, Bibi Sirleaf alikana kuwahi kuwa mwanachama wa kundi lililoongozwa na Charles Taylor wakati wa vita kabla ya Taylor kuwa rais wa Liberia kati ya 1997 na 2003. Lakini Bibi Sirleaf aliiambia tume ya ukweli na maridhiano, kwamba alikutana na Taylor mara kadhaa wakati wa migogoro kadhaa ya nchi hiyo na pia alisaidia kukusanya fedha kumsaidia alipokua akijiandaa kumuangusha Doe mnamo miaka ya 1980.

Tume hiyo ya ukweli na maridhiano imeorodhesha majina kiasi ya manane ya wababe wa kivita ambao imesema wanapaswa kufunguliwa mashitaka kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu mbele ya mahakama maalum nchini Liberia. Hao ni pamoja na Charles Taylor na Prince Johnson ambaye kwa sasa ni mjumbe wa baraza la Seneti.

Charles Taylor Liberia Prozess Den Hagg
Rais wa zamani Charles Taylor naye atajwa kwenye orodhaPicha: AP

Taylor aliliongoza kundi la National Patriotic Front of Liberia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambao Doe aliangushwa na kuuawa na kundi jengine lililojitenga na Taylor likiongozwa na Johnson. Sirleaf alipigania uchaguzi na kushindwa na Taylor 1996, lakini Liberia ikaingia tena katika vita miaka saba baadae.

Bibi Sirleaf aliyeingia madarakani 2006 baada ya kushinda uchaguzi wa kidemokrasi hakutamka lolote hadi sasa kuhusiana na ripoti hiyo, lakini tayari wengine wamezungumza. Mbabe wa zamani wa kivita Johnson kwa mfano anasema atafanya kila liwezalo kuzuwia jaribio lolote la kumshitaki, akiongeza kwamba ripoti hiyo ni "kichekesho," kwani imeshindwa kuwataja wengine kadhaa waliohusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Saah Gborlie aliyekua Naibu mkurugenzi wa polisi wakati wa utawala wa Charlses Taylor amesema, ripoti hiyo imeandaliwa kuwafurahisha wale waliokua na ushawishi mbele ya tume hiyo ya ukweli na maridhiano. Gborlie akasema " watakaonijia basi waje na saga mawe, siendi kokote."

Charles Taylor tayari anakabiliwa na mashitaka 11 ya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binaadamu kutokana na kuwaunga mkono wapiganaji wa Revolutionary United Front-RUF-nchini Sierra Leone wakiati wa vita vya kiraia 1991 hadi 2001,akizuiliwa katika mahakama ya kimataifa mjini The Hague. Kabla ya kukamatwa alikwenda uhamishoni Nigeria 2003 baada ya kupatikana makubaliano yaliomaliza vita nchini mwake Liberia.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman

Mhariri: Sekione Kitojo