Ripoti ya Tume yazua maoni mseto Tanzania
23 Aprili 2026
Kwa upande wake chama cha upinzani CHADEMA kilichosusia uchaguzi huo wa mwaka jana kimesema kinaendelea kujiweka kando na tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu na kwamba hatua hiyo imesimama katika misingi yake ya awali.
CHADEMA kilijiweka kando na uchaguzi huo kikishinikiza kufanyika kwanza mageuzi katika mifumo ya katiba na uchaguzi kwa madai kwamba mifumo ya sasa inabinya uchangamufu wa kidemokrasia.
Akizungumzia matokeo yaliyotolewa na tume hiyo iliyofanya kazi kwa siku 153, Mkurugenzi wa mambo ya nje wa chama hicho, John Kitoka amesema bado chama hicho hakijarudi nyuma kuhusu msimamo wake wa kutoitambua tume hiyo.
Ameiambia DW kuwa CHADEMA haioni sababu kuiunga mkono ripoti hiyo na kwamba baadhi ya hoja zilizotajwa na tume yenyewe zinaonekana kwenda kuwabana waathirika wa matukio ya Oktoba 29.
Wakati Chadema ikiweka msimamo wake juu yaripoti ya tume hiyo, chama kingine cha upinzani ACT Wazalendo kimesema ni mapema mno kuanza kuijadili ripoti hiyo kabla chama chenyewe hakijaanzisha vikao vyake vya ndani kujadiliana hali jumla ilivyo.
Katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu ameeleza yeye binafsi wale chama chake hakiweza kuwa na kauli yoyote wakati huu kukiwa hakujafanyika vikao vyovyote tangu kutolewa kwa ripoti hiyo.
Amesema na hapa namnukuu " Siwezi kuwa na maoni kwa sasa. Mambo mazito kama haya huwa tunaketi kama chama kutafakari na kuongea,” mwisho wa kumnukuu.
Ama, kituo cha sheria na haki za binadamu kimeonyesha kusikitishwa kwake kutokana na maoni yaliyoibuliwa katika ripoti hiyo na kueleza kwamba tume hiyo ilipaswa kumaliza mchakato wote na siyo kutoa mapendekezo ya kuundwa kwa tume nyingine za kiuchunguzi.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Anna Henga amesema hatua ya tume hiyo kupendekeza kuundwa kwa tume nyingine ya uchunguzi kumeibua mkanganyiko wa mambo.
Tume hiyo iliyoanza kufanya kazi tangu Novemba 20 imependekeza kuundwa kwa tume nyingine tatu kufuatilia mapandekezo yake, tume ambazo ni pamoja na itakayofanya uchunguzi wa makosa ya tume ya maridhiano na ile itakayosimamia mchakato wa uandikaji wa katiba mpya, ikipendekeza mchakato huo uwe umekamilika mwaka 2029, ikiwa mwaka mmoja kabla ya kuanza kwa mchaka mchaka mwingine wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.
Ama kituo hicho kimehoji pia kuhusu mlolongo wa tume zinazoendelea kuundwa katika wakati baadhi ya tume hizo maoni yake yakiendelea kusalia makabatini.
Bado kumekuwa na maoni mchanganyiko baada ya kutolewa ripoti ya tume hiyo ingawa yenyewe imesema kuwa hivi karibuni itakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya mambo yaliyoibuliwa.