Rais Trump aakhirisha kuishambulia Iran
23 Machi 2026
Rais Donald Trump amesema,Marekani imefanya mazungumzo mazuri na yenye tija na Iran na kwahivyo ametoa agizo la kuakhirisha kwa muda wa siku tano, mashambulizi ya kijeshi yaliyopangwa dhidi ya mitambo na miundo mbinu ya nishati ya Iran.
Msimamo huo mpya wa Trump, aliouandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth, umekuja saa chache kabla ya kumalizika muda wa saa 48 alizotowa siku ya Jumamosi kuitaka Iran ifungue kikamilifu mlango bahari wa Hormuz.
Marekani na Iran zatishia kushambulia miundombinu muhimu
Hata hivyo Tehran imeyapinga madai ya kiongozi huyo, juu ya kufanyika mazungumzo ya pande mbili ya kumaliza vita vilivyoanzishwa na Marekani na mshirika wake Israel, na haijafahamika ikiwa kuna hatua yoyote iliyopigwa kuhusu suala la kufunguliwa mlango bahari wa Hormuz.
Tangazo la kiongozi huyo wa Marekani limetolewa baada ya Iran kutoa kitisho cha kutaka kuishambulia mitambo ya nishati ya Israel pamoja na ile ya kusambaza nishati kwenye kambi za marekani kwenye eneo la Ghuba, ikiwa itashambuliwa.