Athari ya mzozo wa Iran kwa mashirika ya ndege ya Afrika
24 Aprili 2026
Mafuta ya ndege, yanayotokana na kerosini iliyosafishwa kutoka mafuta ghafi, ndiyo yanayotumiwa na mashirika mengi ya ndege duniani. Lakini tangu kuzuka kwa mzozo wa Iran, bei ya mafuta hayo imeongezeka maradufu katika masoko ya kimataifa, na kusababisha upungufu wa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Dominick Andoh, mshirika mkuu wa Aviation Ghana, jukwaa la habari za safari za ndege mtandaoni, ameiambia DW kwamba hali hiyo imeathiri moja kwa moja mashirika ya ndege barani Afrika, ambayo sasa yananunua mafuta kwa bei ya juu zaidi.
Wasiwasi kuhusu usalama wa nishati pia umechochea kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Kufikia Jumatano, mafuta ghafi aina ya Brent yalikuwa yakiuzwa dola 98 kwa pipa — ongezeko la zaidi ya asilimia 30 tangu vita vilipoanza.
Wachambuzi wanasema hofu ya kuvunjika kwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, pAfrikaamoja na kukamatwa kwa meli ya Iran na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, imechangia hali hiyo.
Andoh anasema mzigo wa ongezeko la bei umehamia kwa abiria, kwani tiketi za ndege zimepanda kwa kiasi kikubwa tangu mzozo huo ulipoanza.
Wasiwasi waongezeka miongoni mwa wafanyabiashara
Hali ya wasiwasi pia imeongezeka miongoni mwa wafanyibiashara wakubwa barani Afrika. Bilionea Aliko ameonya kwamba mashirika mengi ya ndege barani Afrika huenda yasiweze kuhimili ongezeko la muda mrefu la gharama za mafuta.
Mbali na mafuta, vizuizi vya anga katika nchi za Ghuba vimesababisha mashirika ya ndege kubadili njia au kufuta safari, jambo linaloongeza gharama na kupunguza ufanisi wa safari. Hali hii imechangia kupanda kwa bei za tiketi za ndege.
Shirika la ndege la Ethiopian Airlines ni miongoni mwa mashirika yaliyoathirika zaidi. Mwezi uliopita, maafisa wake walieleza kuwa shirika hilo linapoteza takriban dola milioni 137 kila wiki kutokana na kufutwa kwa zaidi ya safari 100 kila wiki.
Ingawa tangazo la kusitisha mapigano lililotolewa wiki iliyopita lilileta matumaini ya muda mfupi, hali ilibadilika haraka baada ya wahusika kukiuka makubaliano.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, baadhi ya mashirika ya ndege ya Afrika yameanza kutumia mikakati mipya. Kenya Airways, kwa mfano, sasa inawapitisha wasafiri wengi wa Ulaya kupitia anga ya Nairobi badala ya njia za kawaida za kupitia nchi za Ghuba.
Licha ya misukosuko hiyo, wadau wa sekta ya anga wanaamini sekta ya anga ya Afrika inaweza kustahimili hali hiyo ikiwa mashirika yatabuni mikakati ya kujilinda — ikiwemo kuhifadhi mafuta ya kutosha na kujikinga dhidi ya mabadiliko ya ghafla ya bei.
Hata hivyo, mkuu wa chama cha mashirika ya ndege IATA, Willie Walsh, ametahadharisha kwamba hata iwapo Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa hii leo, itachukua miezi kadhaa kurejesha upatikanaji wa mafuta katika kiwango cha kawaida.