1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto asisitiza safari yake ya Marekani ilifadhiliwa

30 Mei 2024

Rais William Ruto wa Kenya amejitetea kuwa safari yake ya kihistoria ya Marekani wa wiki iliyopita iligharimu shilingi milioni 10 pekee za Kenya. Haya yamejiri kwenye ibada ya taifa ya 21.

https://p.dw.com/p/4gSwG
Rais wa Kenya William Ruto na mwenzake wa Marekani Joe Biden
Rais wa Kenya William Ruto na mwenzake wa Marekani Joe Biden ( Picha ni wakati wa ziara ya Rais Ruto nchini Marekani )Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Ibada hiyo ilianza kwa pambio na kuwaleta pamoja viongozi wa serikalini. Mbunge wa South Mugirango Sylvanus Osoro aliyepia kiranja wa chama tawala bungeni alitumia fursa hiyo kuonyesha weledi wake wa muziki.

Pindi baada ya kupanda jukwaani, Rais William Ruto wa Kenya alijitetea kuwa safari yake ya nchini Marekani ilipata wafadhili waliomkodishia ndege ya binafsi kwa bei nafuu.

”Nilipofahamishwa kuwa ndege ya bei rahisi zaidi ni milioni 70… niliwaambia wahusika wanikatie tiketi Kenya Airways. Wandani wangu waliposikia Nina Safiri na ndege hiyo wakaniuliza bajeti yangu. Nikawaeleza milioni ishirini wakaniambia lete kumi utapata usafiri. Nitazameni wakenya. Lazima niwe mfano kwenu .” Alisema.

Rais Ruto wa Kenya anaendelea kuusisitizia umuhimu wa kujifunga ukaja na kubana matumizi kwa manufaa ya baadaye.

Soma pia:Marekani, Kenya zatazamia kuimarisha uhusiano wa kibiashara

Wakati huohuo, naibu wake Rigathi Gachagua alijitenga na tetesi zinazoashiria kuwa kuna sintofahamu kati yake na rais Ruto. Badala yake alisimulia jinsi Rais Ruto alivyomshika mkono mkewe Rachel walipokuwa ziarani Marekani na kwamba sio utamaduni wa Kenya.

”Nilimuuliza waziri mkuu wetu Musalia iwapo hata yeye kwake analazimika kumshika mkono mkewe kama tulivyoshuhudia akifanya rais wetu alipokuwa Marekani. Naye alinijibu kuwa huku kwangu ndio balaa. Hata hivyo,nitakapotumwa kwenda Marekani nitamshika mke wangu Dorcas mkono muda wote ntakaokuwa kwenye ardhi ya kigeni.

Nidhamu ndio nguzo ya UDA

Kuhusu mzozo wa kisiasa kwenye chama tawala cha United Democratic Alliance, UDA,Katibu mkuu wake Cleophas Malala alisisitiza kuwa nidhamu sharti ichukue usukani.

Maoni na matarajio ya Wakenya kwa utawala wa William Ruto

Chanzo cha mzozo huo kimemuweka naibu wa rais Rigathi Gachagua kwenye jukwaa la malumbano na utengano katika eneo la Mlima Kenya katika siku za hivi karibuni.

Soma pia:Marekani na Kenya kuimarisha zaidi ushirikiano

Yote hayo yakiendelea,waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia Tamrat Layne aliyekuwa mgeni mashuhuri kwenye ibada hiyo ya taifa amewatolea wito viongozi wa Kenya kukumbatia imani alipokumbushia jinsi aliishi kwa miaka 3 na familia yake kwenye kambi ya wakimbizi mjini Nairobi miaka 24 iliyopita. Tukio hilo lilimvunja moyo na nusura limchoshe nafsi.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ya taifa wamekuwa na mitazamo mbalimba, Sabina Chege ni mbunge wa viti maalum na anasisitiza umuhimu wa imani.

”Tusipoteze Imani. Tujiamini. Tujipende hata tusipoafikiana. Lazima tujizuwie na kuwasikiliza wananchi." Alisema.

Imepita miaka 21 tangu ibada hiyo ya taifa kuanza kufanyika Kenya.