Trump, Starmer kujadili uwekezaji na masuala ya kimataifa
18 Septemba 2025
Mazungumzo ya Rais Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer yanatarajiwa kujikita zaidi kwenye masuala ya kigeni kuliko changamoto za ndani zinazoyakabili mataifa yao. Wawili hao watasherehekea tangazo la uwekezaji wa dola bilioni 205 za Kimarekani nchini Uingereza.
Mikataba katika sekta za teknolojia, nishati na sayansi inayotarajiwa kusainiwa na viongozi hao itasaidia kuhuishwa kwa kile kinachoonekana kuwa uhusiano maalumu kati ya Uingereza na Marekani suala ambalo Waziri Mkuu Starmer amekuwa akilipigania tangu Trump alipoingia mamlakani mwezi Januari.
Moja ya mikataba hiyo kwa mfano ni wa ustawi wa teknolojia unaotajwa kufanya uwekezaji mkubwa wa makampuni ya Marekani ili kusaidia uwezo wa teknolojia ya Akili Mnemba nchini Uingereza.
Starmer na Trump pia watafanya mkutano na waandishi wa habari ambapo huenda wakajikuta wakitakiwa kujibu maswali magumu juu ya kashfa ya mhalifu wa mashambulizi ya kingono Jeffrey Epstein aliyefia gerezani nchini Marekani.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Waziri Mkuu wa Uingereza alilazimika kumfuta kazi balozi wake nchini Marekani Peter Mandelson, baada ya taarifa za ushirika wake wa karibu na Epstein kubainika. Maswali kuhusu Epstein yaliibuka pia katika ziara ya Trump ya mwezi Julai mjini London.
Ushuru, mizozo ya Ukraine, Urusi na Mashariki ya Kati huenda vikagusiwa
Mkutano wa wawili hao unaibua pia matumaini kuwa huenda kukawa na makubaliano yanayodhamiria kupunguza ushuru wa bidhaa za chuma za Uingereza zinazoingizwa Marekani.
Viongozi hao huenda wakawa na mjadala mgumu kuhusu mizozo ya Mashariki ya Ukraine na vita kati ya Urusi na Ukraine. Starmer amekuwa akibeba jukumu kubwa katika juhudi za Ulaya za kuimarisha msaada wa Marekani kwa Ukraine.
Kwa upande wake Trump, bado hajatoa sauti kali ya kuiwekea Urusi vikwazo kwa kurudisha nyuma juhudi za mazungumzo ya kutafuta amani.
Kuhusu Mashariki ya Kati, Waziri Mkuu wa Uingereza amechelewesha mipango yake ya kuitambua Palestina kama taifa hadi Trump atakapomaliza ziara yake. Madhumuni, ni kuepuka kutofautiana waziwazi kuhusu hilo, kwa mujibu wa gazeti la Times.