1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Donald Trump akanusha kumkosoa Theresa May

Zainab Aziz
13 Julai 2018

Katika mkutano na waandishi wa habari Trump alirudia mara kadhaa kuusifu uongozi wa Theresa May na kumtaja kuwa ni "mwanamke ngangari" nalikanusha kumkosoa May katika mahojiano na gazeti la The Sun.

https://p.dw.com/p/31Q4V
Großbritannien PK Donald Trump und Theresa May
Picha: Getty Images/J. Taylor

Viongozi hao walikutana saa chache baada ya Rais Trump kufanya mahojiano na gazeti la The Sun ambapo alisema mipango ya Bibi May kuhusu mahusiano ya baadaye kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya huenda yakauwa matumaini yake ya kufanya biashara na Marekani.

Katika mahojiano hayo Trump pia alitoa kauli zilizoulaumu mpango wa Brexit wa bibi May, alimkosoa Meya wa London Sadiq Khan na wala hakusita kumwagia sifa waziri wa mambo ya nje wa zamani  Boris Johnson, aliyejiuzulu mnamo wiki hii kwamba ni kiongozi wa Uingereza wa baadaye. Hata hivyo, Rais Donald Trump aliwaambia waandishi hao wa habari na kusisitiza kwamba hakumkosoa waziri mkuu wa Uingereza wakati wa mahojiano na gazeti hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa Uingereza Theresa Ma
Rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Rais huyo wa Marekani na Waziri Mkuu May walionesha maoni tofauti juu ya suala la wahamiaji wanaokuja barani Ulaya. Trump amesema suala la uhamiaji limefikia pabaya sana katika bara Ulaya kiasi cha kubadilisha utamaduni wa bara hilo. Kwa upande wake, Waziri Mkuu Theresa May amesema Uingereza inajivunia historia yake ya kuwakaribisha watu kwenye nchi yake, na uhamiaji umeleta mazuri kwa Uingereza kwa sababu watu wa asili tofauti wamechangia mengi kwa jamii ya nchi hiyo ingawa ni muhimu kuwa na sheria ikiwa ni pamoja na sheria za uhamiaji.

Waandamanaji wanaopinga ziara ya Trump nchini Uingereza
Waandamanaji wanaopinga ziara ya Trump nchini UingerezaPicha: Reuters/Y. Herman

Mchana wa leo maandamano kupinga ziara ya Rais wa Marekani nchini Uingereza yaliongezeka. Watu kadhaa walianza kukusanyika kutoka sehemu tofauti kuelekea katikati ya jiji la London kuanzia mapema mchana wa leo tayari kabisa kushiriki kwenye maandamano hayo, makundi yaliyoombwa kushiriki ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, wanaharakati wa haki za binadamu na vikundi vya dini. Maandamano zaidi yamepangwa kufanyika Windsor, ambako rais Trump na mkewe watamtembelea malkia Elizabeth wa Uingereza na pia huko Scotland, ambako Trump anapanga kufanya mapumziko mwishoni mwa wiki kwenye kimoja kati ya viwanja vyake vya golf.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef