1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Leo XIV aongoza misa Angola atoa mwito wa matumaini

19 Aprili 2026

Maelfu ya watu wamehudhuria misa kubwa ya wazi iliyoongozwa na Papa Leo XIV katika eneo la Kilamba lililo nje ya mji mkuu wa Angola, Luanda. Karibu watu 100,000 walihudhuria misa hiyo ya kwanza ya Papa nchini Angola.

https://p.dw.com/p/5CRly
Angola Luanda 2026 | Papa Leo XIV katika ziara nchini Angola
Papa Leo XIV ziarani nchini AngolaPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani ameuhimiza umati kutazama mustakabali wa taifa la Angola kwa matumaini katika mwanzo mpya kwa taifa hilo ambalo bado limeathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 27 ambavyo vilimalizika mwaka 2002.

Papa Leo alisafiri hadi Angola siku ya Jumamosi, ikiwa ni awamu ya tatu ya ziara yake katika nchi nne za Afrika ambako amelaani ufisadi na uporaji wa rasilimali za bara hilo.

Angola Luanda 2026 | Papa Leo XIV
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo XIVPicha: Alberto Pizzoli/AFP

Angola ni nchi mojawapo kati ya wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika na ina utajiri wa rasilimali kama vile almasi lakini umaskini na ukosefu wa usawa vimeshamiri nchini humo. Karibu theluthi moja ya idadi ya watu milioni 36.6 wanaishi katika umaskini, kulingana na Benki ya Dunia. Takwimu rasmi zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watu nchini humo ni vijana, walio na umri wa wastani wa miaka 23.

Muda mfupi baada ya kuwasili, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alikutana na Rais Joao Lourenco na maafisa wengine wa serikali ambapo amekemea mateso wanayoyapata watu na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na unyonyaji uliokithiri wa rasilimali asilia.

Papa Leo XIV atasafiri kilomita 110 kwa helikopta kutoka mji wa Kilamba hadi kwenye mji wa Muxima, eneo takatifu kwa waumini wa kanisa katoliki, ambako lipo kanisa kongwe lililojengwa miaka 300 iliyopita. Kanisa hilo liko mbele ya mto ambao hapo awali ulikuwa njia kuu ya biashara ya watumwa.

Kanisa hilo, lenye sanamu ya Bikira Maria inayojulikana kama "Mama Muxima", kwa maana ya mama wa upendo, huwavutia takriban mahujaji milioni mbili kila mwaka.

Kulingana na viongozi wa kidini, kanisa hilo liilijengwa na walowezi wakoloni wa Angola ambao ni Wareno kwa ajiili ya kuwabatiza watumwa kabla ya kusafirishwa mtoni hadi kwenye bahari ya Atlantiki na kuendelea na safari hadi kwenye bara la Amerika na kwenye visiwa vya Karibik.

Kanisa hilo ni eneo maarufu zaidi la Wakatoliki nchini Angola, hata hivyo historia yake inaashiria jukumu la Kanisa Katoliki katika biashara ya utumwa na baadhi ya wasomi wanaelezea kwamba ubatizo wa kulazimishwa wa watumwa ni jambo ambalo Vatican inaendelea kukataa kulitambua kikamilifu na kuomba radhi.

Angola Luanda 2026 | Papa Leo wa XIV na Rais wa Angola João Lourenço
Kushoto mbel: Papa Leo wa XIV. Kulia Rais wa Angola João LourençoPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Anthea Butler, msomi katika Chuo Kikuu cha Oxford amesema Wakatoliki wengi waafrika weusi ni waumini wa kanisa katoliki kwa sababu ya utumwa kutokana na "Code Noir," iliyohitaji watumwa walionunuliwa na wamiliki Wakatoliki kwanza wabatizwe kanisani.

Amesema kwa Wakatoliki, ziara ya Papa Leo, kwenye eneo takatifu la Muxima ni wakati muhimu wa uponyaji.

Papa Leo alianza ziara yake barani Afrika nchini Algeria siku ya Jumatatu, kisha akaelekea Cameroon na baada ya ziara yake ya nchini Angola, atasafiri hadi Guinea ya Ikweta, kituo chake cha mwisho cha safari barani Afrika.