Kenya huenda ikaufungua tena mpaka wake na Somalia
25 Februari 2026
Kwa zaidi ya miaka 10, juhudi za kuufungua mpaka wa Kenya na Somalia zimekuwa zikiendelea japo mara kwa mara, zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na vitisho vya kiusalama.
Mwezi Mei mwaka 2023, mataifa hayo mawili yalikuwa yameafikia makubaliano ya kufungua mpaka huo ila Kenya ilibadilisha msimamo wake miwezi miwili baadaye kufuatia mauaji ya raia wake watano na polisi wanane karibu na mpaka wake na Somalia,mashambulizi yenyewe yakihusishwa na kundi la wanamgambo la Alshabab.
Mbali na maswala ya mpaka huo, Kenya na Somalia zimekuwa kwenye mzozo wa muda mrefu wa umiliki wa eneo la bahari ya Hindi linalodhaniwa kuwa na madini ya mafuta na gesi yenye urefu wa kilomita 680.
Nini kilichangia mpaka kufungwa?
Sababu kubwa iliyochochea kufungwa kwa mpaka huo,ilikuwa ni usalama huku wakazi sasa wakiunga mkono tangazo la kufunguliwa kwake na kuzitaka mamlaka ya mataifa hayo mawili kuzidisha doria mpakani.
Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi nchini Somalia Ahmed Khadar,amesema,ushirikiano kati ya taasisi za mpakani hasa kuhusu taratibu za uhamiaji itasaidia kurejesha huduma za forodhani.
Khadar aliiambia DW kwamba,hapo awali ushirikiano wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili "ulikuwa mdogo sana, kutokana na udhaifu wa serikali ya Somalia na kwamba,wakati mwingine Somalia haikuwa na serikali kabisa.”
Rais Ruto katika tangazo lake,alisema kikosi maalum cha walinda usalama kutoka vitengo mbalimbali vitahusika kulinda eneo hilo sawia na kuongeza idadi ya polisi mpakani humo.
Kwa mujibu wa mfanyibiashara Mohamed Aden Ali kutoka Beled Hawo,Somalia,Mpaka huo ungefunguliwa hata kabla ya mwezi Aprili kwa kuwa itaimarisha biashara zao.
Kufunguliwa kwa mpaka kunatoa matumaini kwa raia wa nchi mbili
Wakazi wa Somalia waliozungumza na DW,wamesema,Kenya na Somalia ni washirika wa karibu kupitia masuala ya kibiashara,elimu,usalama na mahusiano ya kijamii.
Aidha, wamesema tangazo la kufunguliwa kwa mpaka huo linakuja wakati jamii kutoka pande zote mbili zinakabiliwa na ukame mkali na hivyo,wanahitaji kusafiri ili kutafuta msaada kutoka pande zote.
Tangu Somalia ilipojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2024,imekuwa ikionyesha nia ya kuongeza ushirikiano na mataifa wanachama na imeanza kutekeleza mfumo wa kupata visa mtandaoni na visa za kupokelewa mara unapofika uwanja wa ndege.
Taifa hilo laPembe ya Afrika pia linajitahidi kuwa kituo cha kitalii huku mji mkuu wa Mogadishu ukianza kuwavutia watalii wengi kinyume na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Wachambuzi tofauti nchini humo,wanasema,wasiwasi wa kiusalama sasa si mkubwa kama ulivyokuwa miaka 10 au 15 iliyopita.
Vikosi vya Umoja wa Afrika, vikiwemo wanajeshi wengi kutoka Kenya, vimefanikiwa kurudisha miji mingi ya Somalia chini ya udhibiti wa serikali.
Al‑Shabab bado inachukuliwa kuwa tishio kubwa katika eneo hilo, ingawa baadhi ya wachambuzi wanadokeza kuwa mashambulizi yao yanapungua.
Al‑Shabab ilifanya mashambulizi mabaya nchini Kenya, yakiwemo shambulio la jumba la maduka la Westgate jijini Nairobi mwaka 2013, na lile la Chuo Kikuu cha Garissa mwaka 2015.
Nchini Somalia, kundi hilo limekuwa likilenga mara kwa mara maeneo ambayo hayako chini ya udhibiti wake, yakiwemo miji kama Mogadishu na Kismayo, kwa kutumia mabomu ya malori na magari yenye kuua watu wengi.