Papa kukutana na Askofu Mkuu Rowan Williams | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa kukutana na Askofu Mkuu Rowan Williams

Papa atakutana na kiongozi huyo wa Kanisa la Kianglikani duniani Askofu Mkuu Rowan Williams katika makaazi yake mjini London, ambapo pia atahudhuria Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu huyo.

default

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto XVI.

Ziara ya kihistoria ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita nchini Uingereza, inaingia siku yake ya pili ambapo hii leo atakutana na kiongozi wa Kanisa la Kianglikana duniani huko London. Baba Mtakatifu atahudhuri Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu Mkuu wa Cantebury, Rowan Williams, katika Kanisa Kuu la Westminster Abbey.

Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita atakutana kwa mazungumzo na Askofu Mkuu wa Cantebury, Rowan Williams, katika makaazi ya Askofu huyo kwenye mji mkuu wa Uingereza, London, ikiwa ni katika kuimarisha uhusiano na Kanisa la Kianglikani. Mwanzoni mwa ziara yake ya siku nne hapo jana, Baba Mtakatifu alikuwa Edinburgh ambapo alilakiwa na Malkia Elizabeth wa Pili. Maelfu ya watu walifurika katika mitaa ya Edinburhg kumpokea na pia walihudhiria katika Ibada ya Misa Takatifu ya wazi iliyofanyika huko Glasgow. Wakati wa Ibada hiyo ya Misa Takatifu Baba Mtakatifu alisema, ''Mtafuteni yeye, mumjue na mumpende. Na yeye atawaweka huru kutoka utumwani na kuwaweka kwenye nuru, na pia atawakomboa na kutoka maisha ya hadaa yanayopendekezwa na jamii ya leo.''

Hata hivyo, ziara hiyo ya Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita inafanyika huku Kanisa Katoliki likiwa limeandamwa na kashfa za mapadri wa Kanisa hilo kuwanyanyasa watoto, kingono. Kutokana na kashfa hiyo kuna wasiwasi kwamba idadi ya watu watakaojitokeza kumuona Baba Mtakatifu itakuwa ndogo ikilinganishwa na ile ya watu waliojitokeza wakati wa ziara ya kichungaji ya Hayati Papa Yohane Paulo wa Pili, mwaka 1982. Lakini polisi wamesema kuwa watu 125,000 walijitokeza jana huko Edinburgh kwa ajili ya kumuona Baba Mtakatifu.

Azungumzia kashfa ya mapadri wa Kanisa Katoliki

Akizungumza na waandishi habari kabla ya kushuka katika ndege hapo jana, Baba Mtakatifu alisema kitendo cha kufichuka kwa kashfa hizo kilimshtua na kumhuzunisha. Anasema ni vigumu kuelewa ni vipi vitendo hivyo vilifanyika ndani ya jumuiya ya mapadri. Baba Mtakatifu alisema uongozi wa Kanisa Katoliki haukuonyesha ujasiri wa kutosha na kufanya maamuzi katika kuchukua hatua muhimu kutokana na kashfa hiyo iliyolitikisha Kanisa hilo katika mataifa mengi ya Ulaya na Marekani.

Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, mwenye umri wa miaka 83, ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kufanya ziara rasmi nchini Uingereza, tangu Mfalme Henry wa Nane alipoachana na imani ya Kanisa Katoliki la Roma mwaka 1534. Ziara hii inafanyika huku kukiwa na mivutano kati ya Wakatoliki na Waanglikani na inafanyika miezi 11 baada ya Baba Mtakatifu kuushangaza ulimwengu wa kidini pale aliposema Kanisa Katoliki liko tayari kuwapokea waamini wa Kianglikani watakaoliasi Kanisa hilo baada ya kukasirishwa na hatua ya Kanisa hilo kuwatawaza wanawake kuwa maaskofu.

Baadae leo au kesho, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kundi la waathirika kumi walionyanyaswa kingono mjini London. Pia atakutana na kiasi wanafunzi 3,000 kabla ya kukutana na viongozi wa kidini. Kabla ya kumaliza ziara yake huko Birmingham siku ya Jumapili, Baba Mtakatifu atamtangaza Mwadhama John Kardinali Henry Newman wa Birmingham kuwa mwenye heri. Kardinali huyo maarufu aliyekuwa muumini wa madhehebu ya Kianglikani, alihamia katika Kanisa Katoliki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 17.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PEP1
 • Tarehe 17.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PEP1
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com