Papa ataka amani ya kudumu Ireland ya Kaskazini | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa ataka amani ya kudumu Ireland ya Kaskazini

Wito huo ameutoa leo alipotoa hotuba yake ya kwanza huko Edinburgh alipokaribishwa na Malkia Elizabeth II.

default

Papa Benedikto XVI, (Kulia) akiwa na Mwana Mfalme wa Uingereza Philip, (Shoto) na Malkia Elizabeth II wa Uingereza.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita ambaye leo ameanza ziara ya kihistoria nchini Uingereza, amezitolea wito pande zote zinazohusika Ireland ya Kaskazini kushirikiana na kujitahidi kuhakikisha amani ya haki na ya kudumu inapatikana. Kauli hiyo ameitoa katika hotuba yake ya kwanza hii leo huko Edinburgh, wakati alipokaribishwa na Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.

Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, ambaye aliwasili hii leo nchini Uingereza kwa ziara ya siku nne, amesema kuwa serikali ya Malkia Elizabeth na serikali ya Ireland pamoja na viongozi wa kisiasa, kidini na kiraia wa Ireland Kaskazini, wamesaidia kuwepo suluhu ya kupatikana amani katika eneo hilo. Baba Mtakatifu alisema anamuhimiza kila mmoja kujihusisha na kuendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana. Mzozo wa Ireland ya Kaskazini, unaojulikana kama mzozo kati ya Wakatoliki wanaopinga utawala wa Uingereza na Waprotestanti wanaopenda kutawaliwa na Uingereza, ulisababisha kiasi watu 3,500 kuuawa. Mzozo huo wa miongo mitatu ulimalizika mwaka 1998 siku ya Ijumaa Kuu baada ya kufikiwa kwa mkataba wa amani. Aidha, Malkia Elizabeth aliipongeza Vatican kwa jitihada zake za kutaka kumaliza mzozo huo wa Ireland ya Kaskazini.

Azungumzia unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto

Kwa upande mwingine, akizungumza na waandishi habari kabla ya kushuka katika ndege, Baba Mtakatifu alisema kuwa Kanisa Katoliki lilipotea katika kuzishughulikia kesi za kashfa za mapadri wa Kanisa hilo kuwanyanyasa watoto kingono. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani alisema kitendo cha kufichuka kwa kashfa hizo kilimshtua na kumhuzunisha. Anasema ni vigumu kuelewa ni vipi vitendo hivyo vilifanyika ndani ya jumuiya ya mapadri. Baba Mtakatifu alisema uongozi wa Kanisa Katoliki haukuonyesha ushujaa wa kutosha na kufanya maamuzi katika kuchukua hatua muhimu kutokana na kashfa hiyo iliyolitikisha Kanisa hilo katika mataifa mengi ya Ulaya na Marekani. Makundi yanayopinga kufanyika kwa vitendo hivyo na waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kingono wamemtaka Baba Mtakatifu kuwalipa waathirika hao kwenda mbele zaidi kwa kuomba msamaha.

Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, mwenye umri wa miaka 86 na raia wa Ujerumani, ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kufanya ziara rasmi, kinyume na ziara za kichungaji nchini Uingereza, tangu Henry wa Nane alipoachana na Roma mwaka 1534. Mtangulizi wake, Hayati Papa Yohane Paulo wa Pili, alifanya ziara ya kichungaji nchini Uingereza mwaka 1982, ziara ambayo iligharamiwa kifedha na Kanisa. Kwa kulinganisha, walipa kodi wa Uingereza wametakiwa kuchangia katika gharama za ziara ya Baba Mtakatifu inayokadiriwa kugharimu Pauni milioni 20. Baadae leo Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya wazi inayotazamiwa kuhudhuriwa na watu 80,000 huko Glasgow.

Maeneo mengine atakayotembelea

Kesho ataelekea London atakapokaa hadi Jumamosi, kabla ya kumalizia ziara yake huko Birmingham kwa kumtangaza Mwadhama John Kardinali Henry Newman wa Birmingham kuwa mwenye heri. Kardinali huyo maarufu aliyekuwa muumini wa madhehebu ya Kianglikani, alihamia katika Kanisa Katoliki. Hata hivyo, ziara hiyo ya Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita inaonekana kukabiliwa na changamoto kutoka kwa wale wanaoipinga kwa madai ya kutokubaliana na sera kadhaa za Kanisa hilo, likiwemo suala la uzazi wa mpango, mapadri wanawake, haki za mashoga na kubwa zaidi kashfa ya kuwanyanyasa watoto kingono iliyofanywa na mapadri wa Kanisa hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 16.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PDt7
 • Tarehe 16.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PDt7
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com