Obama: Silaha za kemikali Syria ni hatari kubwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama: Silaha za kemikali Syria ni hatari kubwa

Rais wa Marekani Barack Obama amesema madai ya kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria ni tukio kubwa na la kutia wasiwasi, lakini amejizuia kutaja hatua zinazoweza kuchukuliwa na serikali yake

Picha zilizotolewa na waasi kama ushahidi wa matumizi ya silaha za kemikali

Picha zilizotolewa na waasi kama ushahidi wa matumizi ya silaha za kemikali

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, ambayo yamerushwa mchana wa leo, Rais Barack Obama amesema kuwa madai kwamba mashambulizi hayo ya silaha za kemikali yamefanywa ni hali ya kutia wasiwasi sana, akasisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kulipa umuhimu unaofaa suala hilo.

Alisema, ''Tulichokiona hakika kinaonyesha kuwa hili ni tukio kubwa, na lenye kuzusha wasiwasi. Tayari tumeanza mashauriano na Jumuiya ya Kimataifa, kupitia Umoja wa Mataifa tunajaribu kutafuta hatua muafaka za kuchukuliwa, na tumeitaka Syria kuwaruhusu wachunguzi wa umoja huo walioko huko kufanya uchunguzi.''

Shaka shaka kuingilia kati

Hata hivyo, katika maelezo yake Rais Obama ameashiria kuwa hayuko tayari kuiingiza moja kwa moja Marekani katika vita vya Syria, kwa hofu ya gharama kubwa inayoweza kujitokeza kifedha, na hali kadhalika maisha ya watu yanayoweza kuangamizwa.

Rais wa Marekani Barack Obama amesema madai ya matumizi ya silaha za kemikali yanatia wasiwasi

Rais wa Marekani Barack Obama amesema madai ya matumizi ya silaha za kemikali yanatia wasiwasi

''Ikiwa Marekani itaingilia kati nchini Syria bila ruhusa ya Umoja wa Mataifa wala ushahidi wa kutosha, yanaweza kuibuka maswali juu ya uhalali wa hatua hiyo kisheria'' amesema Obama, na kuongeza kuwa uungwaji mkono wa nchi nyingine kwa hatua hiyo ni suala jingine ambalo lazima litiliwe maanani.

Obama amesema kwamba dhana kuwa Marekani peke yake inaweza kutatua mgogoro wa Syria wenye unaoambatana na matatizo makubwa za kimadhehebu na kikabila, ni kupotosha ukweli wa mambo.

Aidha, Rais Barack Obama amemtaka rais wa Syria Bashar al-Assad kutoa ushirikiano kamili na wachunguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, lakini akatoa tahadhari kuwa hana imani kuwa wito huo utaitikiwa.

Urusi yawatuhumu waasi

Katika kile kinachoonekana kuwa utupianaji wa lawama, Urusi imesema kuwa waasi wa Syria ndio wanaokwamisha wachunguzi hao wa silaha wa Umoja wa Mataifa kufika eneo ambako imedaiwa silaha za kemikali zilitumiwa.

Wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa tayari wako mjini Damascus

Wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa tayari wako mjini Damascus

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo imewashutumu waasi ambao ndio wanaothibiti eneo hilo la mashambulizi, kukwamisha kwa makusudi uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu madai yao. Hali kadhalika, katika tangazo hilo la wizara yake ya mambo ya nchi za nje, Urusi imelaani miito ya matumizi ya nguvu dhidi ya serikali ya Syria kutokana na madai hayo kuwa imetumia silaha za kemikali.

''Kutokana na wimbi jipya la propaganda dhidi ya Syria, tunaamini kuwa shinikizo linalowekwa na baadhi ya nchi za Ulaya kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha matumizi ya nguvu, halikubaliki''; limesema tangazo hilo.

Urusi imesema picha zinazoonyeshwa kama ushahidi kuwa serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali, ziliwekwa hata kabla ya tukio hilo kuripotiwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com