Nigeria: Biashara ya mafuta yazorota | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Nigeria: Biashara ya mafuta yazorota

Angola huenda ikachukua mahala pa Nigeria katika biashara ya mafuta

default

Mfanyikazi wa kampuni ya mafuta ya Shell katika jimbo la Niger Delta nchini Nigeria


Nigeria ambayo imelazimika kufunga zaidi ya nusu ya vinu vya mafuta nchini humo huenda ikapoteza nafasi yake ya kuwa nchi inayouza mafuta mengi zaidi Africa.


Hii ni kufuatia mashambulio ya mara kwa mara katika vinu hivyo na pia migomo ya wafanyikazi.


Nigeria inapoteza zaidi ya nusu ya pato lake katika biashara ya mafuta kutokana na wanamgambo wanaopigana ili mafuta hayo yaelekezwe katika maeneo yao na pia wezi wanaoyaiba na kuyauza kimagendo.


Hasara hiyo inaikumba Nigeria wakati bei za mafuta zimefikia kilele.


Tatizo hilo limeshukisha uzalishaji wa mafuta nchini humo hadi mapipa milioni moja na laki tatu kwa siku kutoka mapipa milioni mbili ambayo nchi hiyo ilikuwa inazalisha hivi majuzi.


Hasara hiyo imekumba kampuni mbili za kimataifa Exxon Mobil na Royal Dutch shell zilizofungwa siku chache zilizopita.


Exxon imepoteza mapipa laki saba na sabini ya mafuta yake ambayo yanaweza kulinganishwa na pato lake la Nigeria kutokana na mgomo wa wafanyikazi.


Wiki jana shell ilisema ililazimika kufunga uzalishaji wa mapipa laki moja na sitini na tisa kwa siku kutokana na mashambulio ya mara kwa mara yanayotekelezwa na wanamgambo katika jimbo la Delta ambalo linazalisha mafuta mengi zaidi nchini Nigeria.


Wanamgambo wanadai shell imefunga uzalishaji wa mapipa laki tatu na hamsini.


Wadadisi wanasema matatizo yanayokumba Nigeria huenda yakaipatia Angola nafasi ya kutawala katika uzalishaji wa mafuta barani Africa.


Wafanyibiashara wanatabiri kwamba kiwango cha mafuta kitakachosafirishwa na Nigeria kitapungua hadi mapipa milioni moja na laki tisa baada ya shughuli ya kupakia kucheleweshwa.


Mpango wa usafirishaji kwa meli nchini Angola unaonyesha nchi hiyo huenda ikasafirisha zaidi ya mapipa milioni moja na laki tisa kwa siku katika mwezi wa mei na juni ilhali mpango kamili wa mwezi wa juni kwa Nigeria haujulikani.


Nigeria na Angola ndio nchi peke barani Africa ambazo ni wanachama wa shirika la nchi zinazosafirisha mafuta OPEC. Kulingana na OPEC Nigeria ina shabaha ya kusafirisha mapipa milioni 2.16 kwa siku.


Nchi hiyo inazalisha mafuta yenye thamani ya juu ambayo ni mepesi na yenye madini machache ya salfa yanayoweza kutumiwa kutengeneza bidhaa zingine kama gasoline na diesel kwa urahisi.


Angola imewekewa shabaha ya mapipa milioni moja na laki tisa kwa siku na shirika la OPEC. Nchi hiyo inazalisha mafuta mazito na yenye madini mengi ya salfa yanayouzwa kwa bei ya chini.


Mike Wittner mkuu wa shirika la kimataifa la utafiti Societe Generale anasema nchi hizo mbili zina wateja tofauti wenye mahitaji tofauti lakini mafuta yenye thamani ya juu yangali yanavutia zaidi.


Hata hivyo wafanyibiashara wanasema wanunuzi wa Nigeria huenda tayari wameanza kutafuta biashara kwengineko kwani kila mwezi usafirishaji unacheleweshwa, mipango ya kupakiwa kwa bidhaa hiyo inabadilishwa mara kwa mara, na hata usafirishaji wake unakatizwa mambo yanayowatatiza wafanyibiashara wa bidhaa hiyo muhimu.


 • Tarehe 01.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Druu
 • Tarehe 01.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Druu
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com