1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Marekani itatoa mwito wa vikwazo dhidi ya Iran

24 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByw

Marekani imesema itatoa mwito Iran iwekewe vikwazo vipya kwa kuendelea kurutubisha madini ya uranium kinyume na matakwa ya Umoja wa Mataifa.

Marekani imetangaza hayo baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia nishati ya nyuklia kutangaza Iran imeongeza vifaa vya kurutubisha madini ya uranium ingawa nchi hiyo iliwekewa vikwazo hapo awali.

Shirika hilo lilitoa taarifa iliyosema Iran imepuuza tarehe ya mwisho iliyowekewa na Baraza la Usalama isimamishe shughuli za urutubishaji.

Taarifa hiyo pia imesema Iran imelikataza shirika hilo kufanya uchunguzi kamili kuhusu mradi wake wa nishati ya kinyuklia.

Iran imekanusha taarifa kwamba imelizuia shirika hilo kufanya uchunguzi na ikasisitiza inazingatia kwa dhati mikataba yote ya kimataifa kuhusu nishati ya kinyuklia.

Mataifa ya magharibi yamekuwa yakishuku Iran kwamba imepania kutengeza silaha za kinyuklia lakini taifa hilo limekuwa likikanusha madai hayo.