1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yasema inatarajia mashambulizi zaidi Ukraine

Iddi Ssessanga
31 Machi 2022

Jumuia ya Kujihami NATO, imesema haioni dalili za vikosi vya Urusi kurudi nyuma nchini Ukraine, na badala yake vinajipanga upya na kuimarisha mashambulizi yake.

https://p.dw.com/p/49Ij7
DW Video Vorschaubild - Stoltenberg: 'Russian units are not withdrawing'
Picha: AFP

Tathmini hiyo ya NATO inakinzana na ahadi iliyotolewa na wajumbe wa majadiliano wa Urusi baada ya mazungumzo nchini Uturuki wiki hii, ya kupunguza pakubwa shughuli za kijeshi za Moscow kaskazini mwa Ukraine, ikiwemo karibu na mji mkuu Kyiv.

"Tunachokiona ni kwamba Urusi inaendelea kutafuta matokeo ya kijeshi ya mzozo wa Ukraine," alisema Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa NATO.

"Ni vyema kwamba mazungumzo yanaendelea, lakini hadi sasa hatujaona mabadiliko ya kweli katika lengo kuu la Urusi, ambalo ni kuwa na matokeo ya kijeshi ya mzozo huo, na wanaendelea kutafuta matokeo ya kijeshi."

Ukraine yawahamisha kutoka mji wa Mariupol uliozingirwa

"Uongo wa Urusi"

Urusi iliahidi wakati wa mazungumzo mjini Istanbul siku ya Jumanne, kwamba ingepunguza operesheni zake karibu na Kyiv na Chernihiv ili kuongeza kuaminiana na kuweka mazingira wezeshi kwa mazungumzo zaidi.

Soma pia: Ukraine yatuma msafara wa mabasi kuondoa watu Mariupol

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy na mataifa ya magharibi yalionesha mashaka kuhusu ahadi hiyo.

Stoltenberg amewaambia waandishi habari Alhamis kwamba Urusi imedanganya mara kwa mara kuhusu nia yake, na kwamba inapaswa kuhukumiwa kwa matendo yake tu na siyo maneno ya viongozi wake.

Katibu Mkuu huyo wa NATO amesema shinikizo linaendelezwa dhidi ya Kyiv na miji mingine, na kwamba wanatarajia mashambulizi zaidi yanayosababisha mateso hata zaidi.

Soma pia: Ukraine: Urusi inaendeleza mashambulizi baada ya kuahidi kusitisha mapigano

Marekani imesema Urusi imeanza kuhamisha chini ya asilimia 20 ya wanajeshi wake, ingawa baadhi walivuka na kuingia Belarus, ambako wanaweza kupatiwa vifaa vingine na kurejeshwa ndani ya Ukraine.

Vita vya Ukraine vyaathiri bei ya bidhaa Tanzania

Urusi yakanusha Putin anapotoshwa

Wakati huo huo, ikulu ya Kremlin imekanusha madai kutoka Washington na London, kwamba rais wa Urusi Vladmir Putin alikuwa anapotoshwa au kuachwa gizani na washauri wake.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, amesema mataifa ya magharibi hayamuelewi Putin, na wala hawaelewi mfumo wa maamuzi wa taifa hilo.

Mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Uingereza Jeremy Fleming, alisema washauri wa Putin walikuwa na uoga wa kumuambia rais huyo ukweli.

Soma zaidi: Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 4

Msemaji wa ikulu ya White House Kate Bedingfield, naye akasema jana kuwa Marekani ina taarifa kuwa Putin anahisi kupotoshwa na jeshi la Urusi, hali iliyopelekea mzozo usiokoma kati yake na uongozi wa jeshi.

Watu 20 wauawa shambulizi la Urusi

Ndani ya Ukraine idara ya usimamizi wa matukio ya dharura imesema watu 20 wameuawa leo kufuatia shambulio la kombora la Urusi dhidi ya makao makuu ya serikali ya mkoa katika mji wa kusini wa Mykolav.

Serikali ya mkoa imeituhumu Urusi kwa kusubiri hadi watu wamewasili kufanya kazi kabla ya kushambulia jengo hilo.

Mazungumzo yamekwama baina ya Ukraine na Urusi

Waziri mkuu wa Italia Mario Draghi, amesema Ulaya inashinikiza kuwekwa ukomo wa bei za gesi na Urusi kwa sababu malipo yake ndiyo yanafadhili vita nchini Ukrane.

Soma pia: Mazungumzo ya amani ya Urusi na Ukraine yameanza Uturuki

Draghi amewaambia waandishi habari wa kigeni leo kwamba, gaharama ambazo Ulaya inalipa haziendani kabisaa na soko la dunia.

Alhamis wachunguzi wa Umoja wa Ulaya wamevamia ofisi za kampuni ya Gasprom nchini Ujerumani, wakishuku kuwa shirika hilo la gesi la serikali ya Urusi limepandisha kinyume cha sheria bei za nishati hiyo barani Ulaya.

Chanzo: Mashirika