1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kupunguza operesheni za kijeshi karibu na Kyiv

Sudi Mnette
29 Machi 2022

Jeshi la Urusi limesema litapunguza kwa kiasi kikubwa operesheni zake za kijeshi karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na mji wa kaskazini,Chernihiv kwa lengo la kutoa fursa ya uwezekano wa makubaliano

https://p.dw.com/p/49BrU
Türkei | Verhandlungen zwischen Russland und der Ukraine in Istanbul
Picha: Turkish Presidency via AP/picture alliance

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Alexander Fomin amesema  hatua hiyo ina lengo la kuongeza hali ya kuaminiana wakati wapatanishi wakikutana ana kwa ana, baada ya duru kadhaa za mazungumzo kushindwa kuzaa matunda yoyote. Ingawa hata hivyo vikosi vya Urusi katika siku za hivi karibuni vinaelezwa kukwama katika jitihada zake za kusonga mbele katika uwanja wa vita.

Mazungumzo ya Urusi yameibua matumani yaliofifia kwamba huenda kukapigwa hatua katika kuelekea kumaliza kampeni ya umwagaji damu katika ardhi ya Ukraine. Naibu Waziri Fomin amesema serikali ya Moscow kimsingi imeamua kupunguza shughuli za kijeshi kuelekea miji ya Kyiv na Chernihiv kwa lengo la kuongeza hali ya kuaminiana na kuweka mazingira ya mazungumzo zaidi baina ya Urusi na Ukraine.

Ishara ya kuondoka kwa majeshi ya Urusi katika miji ya Kyiv na Chernihiv

Ukraine Krieg | Russland deutet Strategiewechsel an
Gari la kivita la Urusi nchini UkrainePicha: Russian Defence Ministry/dpa/picture alliance

Jeshi la Ukraine limeonesha kubaini kuondoka kwa majeshi hayo katika maeneo ya karibu na Kyiv na Chernihiv, Ingawa wizara ya Ulinzi ya Marekani, imesema imeshindwa kuhakiki taarifa hiyo.

Mshauri wa rais wa Ukraine alisema mkutano huo wa leo huko Istanbul ulilenga katika kufanikishwa usitishwaji wa mapigano na dhamana ya kiusalama kwa Ukraine masuala ambayo kwa wakati wote yamekuwa kitovu cha mazungumzo yasiyofanikiwa ya kipindi kilichopita. Mevlut Cavusoglu ni waziri wa mambo ya nje wa Uturuki."Katika mkutano huu uliofanyika leo, tumeshuhudia hatua fulani zimepigwa. Awali mlizisikia kauli za wajumbe. Makubaliano na maelewano yamefikiwa katika baadhi ya masuala. Hatua za maana zaidi zimefikiwa leo tangu kuanza kwa majadiliano. Yale masuala magumu yatapelekwa katika ngazi za juu."

Akizungumza pia muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo kiongozi wa Ujumbe wa Urusi katika mazungumzo hayo, Vladimir Medinsky aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo ya safari hii yamekuwa yenye tija. Na kuongeza kuwa taifa lake lipo tayari kuchukua hatua za kijeshi na kisiasa kupunguza mzozo huo.

Urusi haiwezi kupinga Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya

Kuhusu mapendekezo ya Ukraine, Medinsky amesema yatafanyiwa tathmini katika siku chache zijazo, kuwasilishwa kwa rais na watayajibu kwa kadri itakavyopaswa. Lakini moja ya hayo ni lile la Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya ambalo Urusi haiwezi kulipinga. Serikali ya Urusi imeaonesha ishara ya kutaka kuendelea kwa mazungumzo hayo.

Kabla ya duru hii ya mazungumzo ya sasa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alisema taifa lake lipo tayari kutangaza kutoegemea upande wowote, kama inavyoshinikizwa na Urusi, na ipo tayari kuafikiana kuhusu eneo ya taifa hilo linalozozaniwa la upande wa mashariki la Donbas, kauli ambayo inaweza kutoa msukumo wa mazungumzo ya upatanishi kwa pande hizo hasimu

 

Vyanzo: DPA/RTR/AP.