1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 4

Lilian Mtono
30 Machi 2022

Shirika la kuhudumia wakimbizi ulimwenguni, UNHCR limesema idadi ya raia wa Ukraine waliokimbia nchini mwao imepindukia milioni nne na wengi miongoni mwao wakikimbilia taifa jirani la Poland.

https://p.dw.com/p/49Enu
Polen ukrainische Flüchtlinge in Warschau
Picha: Str/NurPhoto/picture alliance

Kulingana na shirika la kuhudumia wakimbizi duniania la UNHCR kasi na ukubwa wa tatizo la wakimbizi wanaokimbia Ukraine havijawahi kushuhudiwa tangu vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Soma Zaidi:Msisahau wahamiaji wengine mnapoisaidia Ukraine; mashirika  

UNHCR, limesema wakimbizi milioni 4,019,287 wamevuka mipaka ya Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari 24, huku zaidi ya milioni 2.3 wakikimbilia Poland. Nusu ya wakimbizi hao inakadiriwa kuwa ni watoto.

Idadi hiyo tayari imepindukia makisio ya awali ya shirika hilo kwamba huenda vita hivyo vingeibua hadi wakimbizi milioni 4.

Ripoti hii inatolewa wakati, baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa likimteua Jaji Erik Mose kuongoza uchunguzi wa uwezekano wa uhalifu wa kivita uliofanywa na vikosi vya Urusi nchini Ukraine

Wafanyakazi wa misaada wanasema idadi ya wakimbizi hata hivyo imepungua katika siku za karibuni wakati watu wengi wakiwa wanasubiri kitakachoendelea kwenye vita hivyo, wakati takriban watu milioni 6.5 wakiwa wakimbizi wa ndani nchini Ukraine.

Vatikanstadt | Papst Franziskus - Ansprache am Petersplatz
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa mwito wa kumalizwa kwa vita nchini UkrainePicha: Gregorio Borgia/AP/picture alliance

Huko Vatican kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amerejea mwito wake wa kumalizwa kwa vita nchini Ukraine. Papa Francis ametoa mwito huo kwa mara nyingine katika hotuba yake ya wiki kwa waumini huku akiwaomba kuanza tena kuomba ili vita hivyo visimamishwe.

"Turudi nyuma kufikiria kuhusu uharibifu unaotokana na vita na kuanza tena maombi ya kukomesha ukatili huu wa vita," alisema Papa.

Tukielekea sasa mjini Geneva, baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa limemteua jaji Erik Mose, raia wa Sweden kuongoza uchunguzi kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine. Mose ni mjumbe wa zamani wa mahakama ya juu kabisa ya Norway pamoja na mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya. Aliwahi pia kuwa rais wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu nchini Rwanda.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, raia 1,179 wa Ukraine wameuawa, 1,860 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye maeneo ya raia.

Taarifa nyingine zinasema kwamba ujumbe wa Ukraine uliofanya mazungumzo na Urusi huko Istanbul wiki hii umabaki nchini humo kwa ajili ya mazungumzo na serikali ya Uturuki juu ya ushirikiano wa kijeshi katika masuala ya ufundi, hii ikiwa ni kulingana na mpatanishi wa Ukraine David Arakhamia.

Uturuki imechukua jukumu la kuwa mpatanishi kati ya Ukraine na Urusi tangu Urusi ilipovamia taifa hilo jirani.

Tizama Zaidi: 

Mashirika: DW/RTRE