1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka wa tano baada ya kimbunga cha Katrina.

30 Agosti 2010

Zaidi ya watu 1,500 waliuawa, wakaazi waliilaumu serikali kwa uzembe.

https://p.dw.com/p/OzKq
Rais Obama ameahidi kwamba utawala wake utawasaidia waathirika wa Katrina.Picha: AP

Rais wa Marekani, Barack Obama akihudhuria kumbukumbu ya mwaka wa tano tangu kutokea kwa kimbunga cha Katrina katika eneo la New Orleans, aliwasifu wakaazi wa mji huo kwa ujasiri wao na kuahidi kusaidia katika ujenzi mpya na ukarabati wa mji huo hadi ‘kazi yote imekamilika’.

Zaidi ya watu 1,500 walikufa katika kimbunga hicho kilichoiharibu kabisa sura halisi katika mji huo ulioko katika jimbo la Louisiana.

Rais Obama alikiri kwamba mji huo unaosifika kwa muziki wa aina ya Jazz, bado unahitaji msaada lakini jitihada za wakaazi zimehakikisha mji wenyewe unashamiri tena.

Bw Obama alisema kwamba kimbunga hicho kilichosababisha maji kuvuka kingo zamjini huo, kiliwasomba wakaazi na makaazi na lilikuwa janga baya ambalo pia lilikuwa kosa la kibinaadamu lililoonyesha aibu kutokana na uzembe wa serikali. Hata hivyo rais Obama aliahidi kwamba eneo hilo ambalo linapambana na athari ya muda mrefu ya baada ya kimbunga hicho, mzozo wa kiuchumi na pigo la hivi maajuzi la kuvuja kwa mafuta katika ghuba ya Mexico, linaweza kuutegemea utawala wake kwa msaada. Aliuambia umati wa watu kwamba utawala wake utasimama bega kwa bega hadi kazi imekamilishwa.

Flash-Galerie 5 Jahre Hurrikan Katrina
Tarehe 29 Agosti 2005. Maji yenye kasi yalivunja kingo za maji.Picha: AP

Tarehe 29 mwezi Agosti mwaka wa 2005, mji huo unaosifika sana kwa muziki na mandhari ya kuvutia, ulivurugika wakati maji yenye kasi yalipozivunja kingo za maji.

Zaidi ya watu milioni 1.4 wakiwemo wakaazi na watalii waliamrishwa kuhama lakini maji yalipofika wengi walikuwa bado hawajaondoka.

Waathirika wengi waliukimbilia uwanja ambao watu 10,000 waliopoteza makaazi walikopiga kambi. Kimbunga hicho kilisababisha hasara hadi katika majimbo ya Mississippi na Alabama na kukata umeme, mawasiliano pamoja na kuyachafua maji ya kunywa.

Utawala wa rais Obama ulisema umetoa msaada wa kuimarisha miundo mbinu pamoja na idara za sheria na afya na pia kufadhili mipango ya kujenga vizuizi vya takriban kilomita 350 vya kiwango cha juu kuliko vile vya awali.

Siku ya kumbukumbu ya miaka mitano tangu kutokea kwa kimbunga cha Katrina, ilikamilika kwa misa iliyofanywa katika jumba la Armstrong mjini humo. Meya wa mji huo, Mitch Landrieu akizungumza katika misa hiyo alisema, lazima wakabiliane na ukweli kwamba katika mwaka wa tano katika karne hii ya 21,siku nne za mihangaiko, ziliandamwa pia vurugu katika barabara za Marekani. Alisema Vizuizi vya kuzuwia maji viliporomoka na serikali ikashindwa kufanya kazi na kwamba ni siku ambayo hawataisahau yakiwa ni matukio yasiyofaa kutokea tena.

Meya huyo alisema janga hili liliwafunza wakaazi wake umuhimu wa ujirani wema na ushirikiano baina ya watu wa asili tofauti.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed