′Muafaka′ wapatikana Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

'Muafaka' wapatikana Berlin

Muungano wa  kihafidhina unaoongozwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel umefikia makubaliano na chama cha pili kikubwa Ujerumani – Social Democrats, ya kuelekea katika mazungumzo rasmi ya kuunda serikali ya muungano

Baada ya zaidi masaa 24 ya mazungumzo, viongozi wa vyama walifikia kimsingi makubaliano ya kuanzisha mazungumzo rasmi ambayo huenda yakapisha katika miezi kadhaa ijayo kuundwa serikali mpya ya taifa hilo kubwa kabisa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya.

Katika mazungumzo hayo ya usiku kucha mjini Berlin, viongozi wa vyama – Merkel wa Christian Democrats pamoja na kiongozi wa washirika wa Merkel katika jimbo la Bavaria Christrian Social Union – CSU Horst Seehofer na kiongozi wa Social Democrats – SPD Martin Schulz – na wajumbe  wao walifikia makubaliano ya pamoja ya muswada wa kurasa 28 ambao utaweka msingi wa kuanzishwa mazungumzo rasmi.

Kuna vizingiti kadhaa ambavyo bado vipo, ikiwa ni pamoja na kura za wajumbe wenye wasiwasi wa SPD na kisha wanachama wa vyama vya wafanyakazi ambao huenda wakapinga uwezekano wa kuundwa tena serikali ya muungano kati ya muungano wa  Merkel na SPD ambao umeiongoza Ujerumani kwa miaka minne iliyopita.

Deutschland PK Sondierungsgespräche in Berlin Seehofer (Reuters/H. Hanschke)

Kiongozi wa chama cha CSU Horst Seehofer

Ujerumani imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu uchaguzi wa Septemba 24 ambao chama cha Merkel CDU kiliishindwa kupata wingi wa kutosha bungeni – kwa sehemu kutokana na umaarufu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wageni cha Alternative for Germany – AfD ambacho kilipunguza mamilioni ya kura za vyama vyote vikuu. Merkel mwanzoni alivigeukia vyama vidogo viwili, Free Democrats na Kijani, kuunda serikali mpya ya muungano ili kuongoza kwa muhula wake wa nne, lakini baada ya mazungumzo hayo kusambaratika mwezi Novemba, akaamua kwa mara nyingine kuzungumza na SPD ambao nao hawakuwa tayari kwa hilo 

Merkel na Schulz waliingia katika mazungumzo hayo jana wakionya kuhusu vizingiti vikubwa vinavyowasubiri, na duru zikasema mambo yaliyotarajiwa kuzusha mdahalo yalihusu uhamiaji, fedha na sera ya afya.

Karl-Rudolf Korte kutoka chuo kikuu cha Duisburg-Essen anasema mazungumzo hayo hayakuwa tu kuhusu muungano, lakini pia taaluma zao. Anahisi kuwa itakuwa ndo mwisho wa viongozi hao watatu kama hawatofanikiwa kuunda serikali ya muungano.

Deutschland Große Koalition Sondierungsgespräche | Martin Schulz, SPD (Getty Images/AFP/T. Schwarz)

Kiongozi wa SPD Martin Schulz

SPD, ambao wanataka kushinikiza kuhusu ajenda yake ya mafao ya ustawi wa jamii, wanadai unafuu mkubwa wa kodi kwa watu wa kipato cha chini na wastani na kuongeza kodi kwa wenye kipato kikubwa, wakati wahafidhina walifanya kampeni na ahadi ya kupunguza kodi kwa kila Mjerumani.

Ili kuzuia umaarufu wa chama cha AfD, kundi la Merkel linataka kuwa na msimamo imara kuhusu uhamiaji kitu ambacho ni kigumu kuushawishi upande wa SPD katika mazungumzo hayo

Muafaka wa muungano mpya unaweza bado kuzuiwa wakati wajumbe wa SPD, na baadaye wanachama wa vyama vya wafanyakazi, watakapopiga kura kuamua kama chama hicho kinaweza tena kuongoza serikali katika kivuli cha Merkel.

Wasiwasi ni mkubwa baada ya SPD kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa Septemba.

Kiongozi wa tawi la vijana wa chama cha SPD Kevin Kuehnert ameapa kuanzisha kampeni ya kitaifa ya kupinga muungano huo mpya kabla ya kuandaliwa mkutano mkuu wa chama mnamo Septemba 21.

Kura za maoni zinaashiria kuwa Wajerumani hawana tena matumaini na muungano mpya wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na SPD.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com