Morocco kupiga marufuku hukumu ya kifo | Masuala ya Jamii | DW | 25.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Morocco kupiga marufuku hukumu ya kifo

Morocco inaendelea kukabiliwa na hali ya wasiwasi kufuatia mauaji mengi yaliyafanywa mbali na hukumu za vifo zilizotolewa na mahakama katika miaka ya nyuma. Lakini watetezi wa haki za binadamu wanalitazama pendekezo la kupiga marufuku hukumu ya kifo kama hatua muhimu itakayowahimiza Wamorocco wengi kushuhudia wanayoyajua kuhusiana na mauaji hayo na kusaidia kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria watuhumiwa.

Mfamle Mohamed VI wa Morocco

Mfamle Mohamed VI wa Morocco

Kuingia madarakani kwa mfalme Mohamed VI mnamo mwaka wa 1999 kulifuatiwa na harakati za kuleta maridhiano kati ya serikali ya Morocco na wahanga wa ukiukaji wa haki za binadamu wakati babake alipokuwa uongozini. Juhudi hii ilituwama juu ya kamati ya usawa na maridhiano iliyosaidia kesi za waathiriwa kusikilizwa na kulipwa fidia.

Kamati hiyo ilikamilisha kazi yake zaidi ya mwaka mmoja uliopita na kutoa ripoti ya mwisho iliyotaka hukumu ya kifo ipigwe marufuku. Vyombo vya habari nchini Morocco vimedokeza pendekezo hilo huenda likaidhinishwa na bunge wakati wa kikao chake cha sasa ambacho kitamalizika mwezi Juni mwaka huu.

Lakini watetezi mashuhuri wa haki za binadamu bado wanakosoa kwamba kuna kesi nyingi za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ambazo bado hazijafichuliwa. Mauaji yaliyofanywa bila hukumu ya vifo kutolewa na mahakama wakati wa utawala wa mfalme Hassan II bado yamebakia kuwa siri kubwa.

Noureddine Gabba, mwanachama wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini Morocco, aliliambia shirika la habari la IPS kwamba maridhiano hayawezi kufanyika nusu nusu. ´Kuna njia moja ya kukamilisha maridhiano nayo ni kusema ukweli wote. Tunahitaji kujua yaliyowapata wahanga,´ amesema Gabba. ´Tunahitaji kuhakikishiwa kwamba haya hayatarudiwa tena,´ akamalizia kusema mtetezi huyo.

Kupigwa marufuku hukumu ya kifo nchini Morocco ni muhimu kujenga taifa linaloheshimu utawala wa kisheria, haki za binadamu na uhuru. Hatua hiyo hatimaye inatarajiwa kufichua ukweli wote uliofichika kwa wakati huu. Huenda ikawasaidia maafisa wa zamani wa ujasusi kufichua habari muhimu kuhusu yaliyotokea wakati wa utawala wa miaka 38 wa mfalme Hassan II.

Maafisa waliowanyonga watu wakijua hawawezi kuhukumiwa kifo huenda wakawa tayari zaidi kusema yaliyotokea na hivyo ukweli wote huenda ukajitokeza.

Utawala wa mfalme Hassan II ulishuhudia wapinzani na watetezi wa demokrasia wakiteswa, kufungwa gerezani na wengi kupotea. Mfano wa kisa cha ukiukaji wa haki za binadamu ni kupotea kwa kiongozi mkuu wa upinzani, Mehdi Ben Barka, mnamo mwaka wa 1965.

Afisa wa zamani wa ujasusi, Ahmed Boukhari, alikiri mnamo mwaka wa 2000 jinsi alivyopanga njama ya kumteka nyara Ben Barka mjini Paris Ufaransa akiwa katika kituo chake cha siri cha ujasusi cha Dar al-Moukri. Hili ni jumba la kifahari lililo katika wilaya ya Souissi katika mji mkuu Rabat. Mawakala waliiiba maiti ya kiongozi huyo wa upinzani na kuingiza kwenye asidi n akuyeyuka bila kuwepo na mabaki yoyote.

Lakini licha ya ushuhuda huo hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi ya mtu yeyote aliyehusika na mauaji mbali na hukumu ya kifo. Serikali ya Morocco mara kwa mara imepuuza miito ya kulifungua jumba hilo la ujasusi na siri zake kwa raia. Ilikataa kutoa ruhusa ya kufanyika maandamano ya amani kuibinya.

Hatua ya serikali kutokuwa tayari kuanzisha uchunguzi wa mauaji nchini Morocco mbali na hukumu ya kifo inaendelea kusababisha uchungu miongoni mwa jamii za waathiriwa huku watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo wakiendelea kuonekana kwenye runinga inayomilikiwa na serikali.

 • Tarehe 25.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHl7
 • Tarehe 25.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHl7

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com