Miaka 17 ya muungano | Magazetini | DW | 04.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Miaka 17 ya muungano

Eti kweli mapatano ya fedha ziada za mshikamano yanastahiki kuendelezwa?

Mada moja tuu ndiyo iliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo:Siku kuu ya Muungano.

Spika wa bunge la shirikisho Lammert akihutubia katika sherehe rasmi za kuadhimisha miaka 17 ya muungano wa Ujerumani,amesema juhudi za muungano na ujenzi mpya wa mashariki zimefanikiwa.Si wahariri wote lakini wa magazeti ya Ujerumani wanaounga mkono hoja hizo.Kuna wanaosifu na wale wanaokosoa pia.Kwa mfano mhariri wa gazeti la KIELER NACHRICHTEN anaandika:

„Mnamo mwaka wa 18 baada ya muungano,mtu anaweza kushuku haja ya kuendelezwa michango ya fedha za „mshikamano“ bila ya kujikuta akiitwa „mpinzani wa muungano.“Kile kilichokua kikiitwa „malipo ziada ya muda kimegeuka kodi ya kudumu ,inayotumika sio tuu kugharimia miradi maalum ya mashariki bali pia kupunguza nakisi ya bajeti ya serikali kuu .Lingekua jambo la maana kama wahubiri wa Schwerin,mbali na kuwashukuru raia kwa kuunga mkono shughuli za kuijenga upya sehemu ya mashariki ya Ujerumani,wangewaambia tarehe pia wanayofikiria kusimamisha „michango hiyo ya mshikamano.“

Gazeti la RHEIN-ZEITUNG la mjini Koblenz lina maoni sawa na hayo na linaandika:

„Tunafurahi kuona majimbo mengi ya ile iliyokua Ujerumani mashariki ya zamani,yanashindana hivi sasa na majimbo ya magharibi.Lakini tusidanganyike kwa fahari ya ufanisi huo,mashariki ya Ujerumani bado kuna mengi ya kufanya.Na magharibi pia kuna maeneo ya shida ambako barabara,shule na miji inahitaji kujengwa upya.Mapatano ya fedha za mshikamano yanahitaji ufanisi mkubwa zaidi na ukaguzi mkubwa zaidi.Na lazma yaambatanishwe na wakati na kutathmini kama fedha hizo ziendelee kweli kumiminwa pekee katika maeneo masikini ya mashariki.Na magharibi jee?

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE la mjini Postdam halioni umuhimu wa kuendelezwa mjadala kuhusu malipo ya fedha za mshikamano.Gazeti linachambua:

„Haijulikani bado kwanini baadhi ya wanasiasa wanahisi siku ya muungano ndio siku muwafak ya kufikiria uwezekano wa kufutiliwa mbali malipo ya fedha za mshikamano.Makadirio ya hali ya maisha katika maeneo ya mashariki sio sababu pekee,kwasababu bado mwanya ni mpana kati ya majimbo ya zamani na yale mepya ya Ujerumani.“

Lawama kali zaidi zimetolewa na gazeti la LANDESZEITUNG la mjini Lüneburg:

„Miaka 17 ya Muungano yamelipatia eneo la mashariki miundo mbinu madhubuti,majengo adimu ya shughuli za utamaduni na viwanda vya kimambo leo.Muhimu zaidi lakini ni zile dosari zilizotokana na muungano:makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yamejipatia uwanja-yanaranda tuu na visa vyao vya kikatili;Chuki dhidi ya wageni na shauku ya hali ya maisha kabla ya ukuta kuporomoka.Miaka 17 haijatosha kufuta mabaki ya wanazi seuze ya utawala wa kiimla wa SED.“

 • Tarehe 04.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7lW
 • Tarehe 04.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7lW
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com