Mgomo nchini Ufaransa waingia siku ya saba | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 20.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Mgomo nchini Ufaransa waingia siku ya saba

Kupamba moto kwa mgomo huo ni shinikizo kubwa zaidi kwa rais Nikolas Sarkozy.

default

Wafanyakazi wa reli wakiandamana mjini Marseilles.

Mamia kwa maelfu ya watumishi wa serikali nchini Ufaransa pamoja na wanafunzi wanashiriki katika mgomo nchini kote leo, wakijiunga na mgomo wa wiki nzima sasa wa wafanyakazi wa sekta ya usafiri

Watumishi wa serikali, wakiwemo waalimu wafanyakazi wa posta na waongozaji misafara ya ndege, wamejiunga wanagoma kwa siku moaja leo, kuunga mkono madai ya nyongeza ya mishahara na kusitishwa mpango wa kupunguza nafasi za ajira.

Hatua yao inaungana na mgomo wa siku saba mfululizo wa wafanyakazi wa sekta ya usafiri nchini kote, ambao umevuruga huduma zote za usafiri wa reli nchini Ufaransa na kuwaacha wakaazi wa mji mkuu Paris katika matatizo ya kila siku kusaka njia za kufika makazini .

Sambamba na hayo, serikali inakabiliwa pia na kampeni ya wanafunzi kupinga sheria inayoviruhusu vyuo vikuu kupata fedha kutoka duru za binafsi pamoja na mahakimu wanaopinga kufungwa baadhi ya mahakama. Yote hayo yamezusha mtihani mkubwa kwa rais Nikoalas Sarkozy kuwahi kukabiliana tangu alipoingia madarakani mwezi Mei mwaka huu.

Mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi uliitishwa kwa sababu ya mpango wa Sarkozy kutaka kufuta utaratibu maalum wa pesheni, ambao wafanyakazi 500,000 wa sekta hiyo na ile ya nishati wamekua wakinufaika nao hadi sasa, ikiwa ni kustaafu miaka miwili na nusu mapema, kuliko wenzao wa sekta nyengine.

Kutokana na mgomo huo Waziri wa fedha bibi Christine Lagarde, anasema shughuli za kijamii zimeathirika na kuugharimu uchumi hasara ya kati ya euro 300 na 400 milioni kwa siku.

Bado kuna matumaini ya uwezekano wa kufikiwa muwafaka baada ya vyama vya wafanyakazi kusema vitashiriki katika mazungumzo na serikali yanayopangwa kesho Jumatano.

Awali serikali ilisema itazungumza tu pale mgomo utakapomalizika, lakini mnamo siku ya Jumapili, waziri wa kazi Xavier Bertrand alisema atahudhuria mazungumzo ya kesho ikiwa kutakua na moyo wa kuwa tayari kurudi makazini.

Hata hivyo serikali imesisitiza kuwa haitorudi nyuma katika mpango wake kuhusiana na mageuzi katika mfumo wa pensheni, lakini mependekeza nyongeza ya mishahara na tija nyenginezo. Utawala wa shirika la usafiri wa reli SNCF umetajka kuwa tayari kuvipa vyama vya wafanyakazi mpango wa fedha wa zaidi ya euro milioni 90, ikiwa vitayakubali marekebisho hayo.

Pamoja na sakata hilo kuendelea, kura za maoni ya wakaazi nchini Ufaransa zinaashiria kwamba kinyume na migomo iliopita nchini humo, safari hii wengi wanaupinga mgomo huu. Utafiti mmoja wapo umegundua kwamba 64 asili mia ya wakaazi wanaunga mgomo mageuzi ya pensheni yaliopendekezwa na serikali na ni 33 tu asili mia ya wakaazi wanaouunga mkono mgomo huo.

 • Tarehe 20.11.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CPUv
 • Tarehe 20.11.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CPUv

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com