Merkel, Hollande wamuonya tena Putin | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel, Hollande wamuonya tena Putin

Huku muda wa mwisho wa usitishwaji mapigano mashariki mwa Ukraine ukikaribia , viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wamemuonya rais wa Urusi juu ya vikwazo vipya iwapo hatawalazimisha wanaharakati kumaliza uasi.

Mazungumzo ya viongozi hao wanne yanaazimia kuumaliza mzozo wa wiki 13 mashariki mwa Ukraine

Mazungumzo ya viongozi hao wanne yanaazimia kuumaliza mzozo wa wiki 13 mashariki mwa Ukraine

Onyo hilo limetolewa katika mazungumzo ya simu ambayo pia yalimshirikisha rais mpya wa Ukraine. Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande wamemueleza rais wa Urusi Vladimir Putin, kwamba anao muda wa hadi leo tu kuwawekea shinikizo wanaharakati wa mashariki mwa Ukraine ambao wanataka kujitenga, kuacha mara moja uasi wao dhidi ya serikali ya mjini Kiev.

Katika ujumbe mkali kutoka kwa viongozi hao wa Umoja wa Ulaya, Putin ameambiwa wazi kwamba iwapo atashindwa kufanya hivyo, upo uwezekano wa nchi yake kuwekewa vikwazo vya pamoja vya nchi zote 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya, na kuutenga mbali kabisa uchumi wa Urusi. Marekani imeahidi kuungana na Ulaya katika kuichukulia hatua Urusi.

Mbinyo mkali na vikwazo zaidi

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Taarifa kutoka Ufaransa zimeeleza kuwa katika mazungumzo yao, Kansela Merkel na Rais Hollande wametilia mkazo umuhimu wa hatua za haraka kurejesha utengamano mashariki mwa Ukraine, kurefushwa kwa muda wa usitishwaji mapigano, na kutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na serikali mjini Kiev. Taarifa hiyo imeongeza kuwa viongozi hao wa Ulaya wamemjulisha rais Putin kwamba matumaini yao ni kuwa matokeo wanayoyatarajia yatapatikana leo Jumatatu.

Hata hivyo, taarifa kutoka Ikulu ya Urusi, Kremlin haikuzungumza masharti hayo ya Umoja wa Ulaya, badala yake imesema kuwa rais Putin, Kansela Merkel na Rais Hollande, kwa pamoja wamemtaka rais mpya wa Ukraine Petro Poroshenko, kutoanzisha tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya wanaharakati wa mashariki mwa nchi yake.

Maelezo tofauti kutoka Moscow

Rais wa Urusi Vladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin

Katika taarifa hiyo Urusi imerudia wito wake wa kuitaka serikali ya Ukraine iridhie mara moja mpango wa Urusi wa kupeleka msaada wa kibinadamu mashariki mwa nchi. Ukraine inashuku kwamba huenda Urusi ikautumia mpango huo kuingiza kimagendo silaha kuwaimarisha waasi.

Tofauti nyingine za kimtazamo kati ya Urusi na Ukraine zimedhihirika kwenye uwanja wa mapambano. Kiongozi wa waasi amesema hawatakubali mazungumzo yoyote na serikali ya Kiev hadi pale itakapokuwa imeondoa wanajeshi wake kutoka eneo la mashariki ambalo linaegemea upande wa Urusi. Naye rais wa Ukraine Petro Poroshenko, ameapa kutokutana na makamanda wa waasi, ambao amesema mikono yao imejaa damu.

Mikono iliyojaa damu

Rais mpya wa Ukraine Petro Poroshenko

Rais mpya wa Ukraine Petro Poroshenko

Hata hivyo, rais Poroshenko amesema kuwa mazungumzo hayo ya jana yataendelea baadaye leo, saa chache kabla ya kumalizika muda wa mwisho wa usitishaji tete wa mapigano ambao ni saa nne za usiku, leo saa ya Ukraine.

Mazungumzo haya baina ya viongozi wa Ulaya na rais Putin yalipangwa Ijumaa iliyopita mjini Brussels, baada ya rais Petro Poroshenko kutia saini makubaliano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya. Mgogoro wa sasa wa Ukraine uliibuka baada ya rais wa wakati huo Viktor Yanukovych kukataa kuyatia saini makubaliano hayo, na badala yake kuisogeza zaidi nchi yake kwa upande wa Urusi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com