Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati.

Benjamin Netanyahu asema Kusitishwa kwa muda ujenzi wa makaazi ya walowezi katika ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan haujafaulu katika lengo lake.

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akutana na Rais Barack Obama mjini Washington.

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akutana na Rais Barack Obama mjini Washington.

Waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, amesema Kusitishwa kwa muda ujenzi wa makaazi ya walowezi katika ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan haujafaulu katika lengo lake la kuwashawishi Wapalestina kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa ajili ya amani.

Lakini, hata hivyo, hakusema iwapo ujenzi wa makaazi hayo utaendelea baada ya muda uliotolewa wa kusitisha ujenzi huo kuisha ifikapo mwezi Septemba.

Akizungumza mwisho wa ziara yake ya siku tatu Marekani, alikokuwa na mkutano na Rais wa nchi hiyo, Barack Obama, Waziri huyo Mkuu alisema kuwa Baada ya uamuzi wa kusitisha ujenzi wa makaazi hayo kwa muda wa miezi kumi, miezi saba tayari imepita na mpaka sasa Wapalestina hawajakubali kufanya mazungumzo ya moja kwa moja ya amani, na kuwa hakuna haja ya kupoteza wakati zaidi.

Katika ziara yake yote, Netanyahu alieleza nia yake ya kukutana na kiongozi wa Palestina kwa mazungumzo hayo ya amani kwani wakati umewadia.

Huku Wapalestina na Marekani wakisema ujenzi wa makaazi hayo ya walowezi katika ukingo wa Maghribi ni kizuizi kwa kupatikana amani, wafuasi wa chama cha Netanyahu cha mrengo wa kulia cha Likud hawajafurahishwa na kusitishwa ujenzi wa makaazi hayo.

Netanyahu ameashiria kuwa yupo tayari kuafikiana na Wapalestina, jambo ambalo huenda lisipokelewe vyema, kisiasa, nchini Israeli.

Katika mahojiano na shirika la habari la CNN, Netanyahu aliahidi kuwa hatima ya maeneo yaliomo katika maeneo ambayo Wapalestina wanadai kuwa yao, ndilo jambo litakalojadiliwa kwanza iwapo Wapalestina watakubali kuendeleza na mazungumzo ya moja kwa moja kutafuta amani.

Wapalestina walisitisha mazungumzo hayo ya amani mnamo mwezi Desemba mwaka 2008 wakati Israeli ilipo anzisha mashambulizi makubwa ya siku 22 katika eneo linaloongozwa na kundi la Hamas la Gaza katika jitihada za kusitisha mashambulizi ya mipaka ya mabomu roketi.

Tangu mwezi Mei pande hizo mbili zimekuwa zikiwasiliana kupitia mjumbe wa amani wa mashariki ya kati wa Rais Obama, George Mitchell ambaye mpaka hivi sasa amefanikiwa kufanya ziara tano za kidiplomasia.

Netanyahu amerudi jana Israeli, na kwa mujibu wa Afisa mmoja wa Israeli amabye hakutaka kutajwa jina, amesema waziri mkuu huyo wa Israel huenda akaelekea Misri wiki ijayo kwa mazungumzo na rais Hosni Mubarak ambaye ni mshawishi mkuu katika jitihada za kupatikana amani katika maeneo hayo.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri: Miraji Othman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com