Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati kuanza | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati kuanza

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ambapo amesema mazungumzo hayo huenda yakaanza katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Rais Hosni Mubarak wa Misri (Kulia) akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu.

Rais Hosni Mubarak wa Misri (Kulia) akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu amesema anatarajia kuwa mazungumzo ya amani ya moja kwa moja kati ya Israeli na Palestina yataanza kaitka kipindi cha wiki mbili zijazo. Wakati huo huo, Rais wa Israeli Shimon Peres jana alikutana na mwenzake wa Misri, Hosni Mubarak katika jitihada za kuyafufua mazungumzo hayo ya amani katika Mashariki ya Kati.

Taarifa zinaeleza kuwa Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu hakuwaambia mawaziri wa chama chake cha Likud kuhusu matarajio hayo, lakini baadae aliliambia baraza zima la mawaziri kuwa mazungumzo aliyoyafanya hivi karibuni yameweka mazingira mazuri ya kuanza tena kwa mazungumzo ya amani ya moja kwa moja kati ya Israeli na Mamlaka ya Palestina. Israeli na Wapalestina walianza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja wakati wa majira ya mchipuko, huku mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell akiwa mpatanishi. Bwana Netanyahu amekuwa akishinikiza kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja, madai yanayoungwa mkono pia na Rais Barack Obama wa Marekani. Lakini Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas amesema mazungumzo ya moja kwa moja hayatafanyika hadi atakapohakikishiwa kuwa Israeli itaachana na shughuli zake za ujenzi wa makaazi ya Walowezi na pia kuhusu suala la mipaka katika taifa la baadae la Palestina.

Katika hatua nyingine, Rais wa Israeli Shimon Peres jana alikutana na mwenzake wa Misri, Hosni Mubarak. Msemaji wa Rais Mubarak alisema kuwa kiongozi huyo alimwambia Rais Peres kuwa kuna haja ya kuanzisha mazingira yanayofaa kwa ajili ya mazungumzo ya moja kwa moja. Kwa mujibu wa msemaji huyo, Suleiman Awad, mazingira hayo yatajumuisha suala la Israeli kuondoa masharti ya Wapalestina kutembea katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Rais Mubarak alimwambia mwenzake kuhusu msimamo wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu uliofikiwa wiki iliyopita kwamba inaunga mkono mazungumzo hayo ya moja kwa moja, lakini endapo madai ya Wapalestina yatatekelezwa ndani ya muda uliowekwa.

Wakati jitihada za kuyafufua mazungumzo ya amani zikiendelea, Israeli imekanusha kuwa mripuko uliotokea Gaza na kuwajeruhi kiasi watu 24 ulisababishwa na shambulio la anga lililofanywa na Israeli. Msemaji wa jeshi la Israeli mjini Tel Aviv amesema nchi hiyo haijahusika na shambulio hilo. Shambulio hilo lilitokea katika nyumba ya Adnan Adaf, kamanda wa juu wa kundi la Hamas katika kambi ya wakimbizi ya Deir el-Balah, kusini mwa Gaza. Awali Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alitoa onyo kali kwa kundi la Hamas ambalo linadhibiti Ukanda wa Gaza, kufuatia mashambulio ya roketi yaliyofanywa mwishoni mwa wiki kutokea Palestina katika maeneo ya Waisraeli. Hakuna kundi lolote la Palestina ambalo limedai kuhusika na mashambulio hayo yaliyotokea Ijumaa iliyopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,DPAE,APE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 02.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OZtk
 • Tarehe 02.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OZtk
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com