1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati kuanza tena Septemba Pili

Kabogo Grace Patricia21 Agosti 2010

Mazungumzo hayo ya ana kwa ana yataanza tena baada ya Palestina na Israeli kuukubali mwaliko uliotolewa na Marekani.

https://p.dw.com/p/Osww
Mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell.Picha: AP

Viongozi wa Kipalestina wameukubali mwaliko wa Marekani wa kuanza tena mazungumzo ya amani ya ana kwa ana na Waisraeli. Uamuzi huo umepitishwa baada ya kushauriana na chama cha PLO na mataifa ya Kiarabu. Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu pia ameukubali mwaliko huo.

Mapema hiyo jana, kundi la pande nne linaloshughulikia amani ya Mashariki ya Kati zikiwemo Marekani, Urusi, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa lilitoa mwito kwa Israeli na Wapalestina kuanza tena mazungumzo ya ana kwa ana tarehe 2 ya mwezi ujao wa Septemba. Katika mkutano na waandishi habari, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema lengo ni kuundwa kwa taifa la Palestina katika kipindi cha mwaka mmoja na kuleta amani katika moja ya mizozo sugu kabisa duniani.

Bibi Clinton alisema mazungumzo hayo yatakayofanyika mjini Washington, Marekani yatajadili masuala yote ya hadhi ikiwa ni pamoja na suala la mipaka ya taifa la baadae la Palestina, hadhi ya wakimbizi wa Kipalestina na mustakabali wa jiji la Jerusalem. Mazungumzo hayo yamekwama kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na madai ya Wapalestina kuwa Israeli isitishe ujenzi wa makaazi ya Walowezi, huku Israeli ikisisitiza kuwa yasiwepo masharti yoyote.