Mawaziri wa EU waidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi
28 Mei 2024Mfumo mpya wa vikwazo ulianzishwa kufuatia kifo cha kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny na unawalenga watu na mashirika yanayohusika na ukandamaziji wa upinzani. Jumla ya watu 19 nchini Urusi wamelengwa wakiwemo maafisa wa idara ya mahakama ya Urusi, waendesha mashitaka wa serikali na maafisa wa usalama waliohusika na kufungwa jela kwa Navalny.
Mkosoaji huyo wa serikali ya Urusi alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa katika jela ya eneo la Siberia mwezi Februari. Kifo chake kinatajwa na wengi kusababishwa na mazingira magumu mikononi mwa mamlaka za Urusi.
Soma pia: Urusi yakemea pendekezo la kutumia mapato ya mali zake zilizozuiwa
Maafisa wa Urusi waliohusika na kushtakiwa kwa mwanaharakati wa haki za binaadamu Oleg Orlov pia walijumusihwa. Bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu duru ya 14 ya vikwazo dhidi ya Urusi kwa vita vyake nchini Ukraine. Kwa mara ya kwanza, sekta ya gesi asilia ya Urusi yenye faida kubwa inazingatiwa.