1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauzo ya silaha yaongezeka Mashariki ya Kati

Isaac Gamba
12 Machi 2018

Mauzo ya silaha katika nchi zinazokabiliwa na migogoro Mashariki ya Kati yameongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita huku Marekani na nchi za ulaya zikisafirisha shehena kubwa ya silaha.

https://p.dw.com/p/2u8b5
Kampfroboter
Picha: picture-alliance/dpa/D. Herrick

Kwa mujibu wa  taasisi  ya kimataifa ya Stockholm  inayohusika na masuala ya amani  ya  SIPRI- mauzo ya silaha katika mataifa ya Mashariki ya Kati yaliongezeka kwa asilimia 103 katika kipindi cha mwaka 2013-2017 kulinganisha na miaka mitano iliyotangulia.

Mtafiti  wa taasisi ya SIPRI, Pieter Wezeman  katika taarifa yake anasema kuongezeka kwa migogoro katika mashariki ya Kati na wasiwasi kuhusu haki za binadamu kumepelekea kuwepo mijadala ya kisiasa ulaya magharibi  na Amerika ya Kaskazni juu ya haja ya kuzuia mauzo ya silaha.

Hata hivyo Marekani na nchi za ulaya zinasalia kuwa wauzaji wakuu wa silaha  na zilisafirisha zaidi ya asilimia 98 ya silaha zilizoingizwa nchini Saudi Arabia anasema mtafiti huyo.

Saudi Arabia inayoongoza kampeni kubwa ya kijeshi dhidi ya waasi wahouthi nchini Yemen imeshuhudia ununuzi wake wa silaha ukiongezeka kwa asilimia 225 katika kipindi cha  kati ya mwaka 2013-2017 kulinganisha na mwaka 2008 hadi 2012.

Saudi Arabia ambayo ni nchi ya pili duniani kuagiza silaha kwa wingi ikitanguliwa na India  wiki iliyopita ilikubali kununua ndege 48 za kisasa za kivita kutoka shirika la BAE  Systems la Uingereza mnamo wakati wanaharakati wa haki za binadamu wakiikisoa  Saudi Arabia kuwa inatumia silaha hizo zilizonunuliwa kutoka nchi za magharibi kuwaua raia wasio na hatia nchini Yemen.

 

Marekani yaongoza kwa kuuza silaha nyingi

Utafiti huo wa SIPRI umezidi kubainisha kuwa Marekani ilidhihirisha kuwa ndio nchi inayoongoza duniani  kwa kuuza silaha nyingi zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ikiuza karibu theluthi moja ya silaha  huku mauzo ya silaha  katika mataifa ya Mashariki ya Kati yakiwa ni nusu ya silaha zilizouzwa kutoka Marekani katika kipindi hicho.

Argentinien Buenos Aires - Konfiszierte Waffen bevor Sie durch Waffenregulierungenzerstört werden
Baadhi ya silaha zinazotumika katika vitaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Marcarian

Kulingana na mikataba iliyosainiwa wakati wa utawala wa rais Barack Obama , mauzo ya Marekani ya silaha katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013- hadi 2017 yalifikia kiwango cha juu kabisa kulinganisha na mauzo ya nchi hiyo yaliyofanyika hadi mwishoni mwa miaka ya 1990.

Mikataba hii pamoja na mikataba mingine mikubwa iliyosainiwa mwaka 2017 inaashiria  Marekani itaendelea kusalia  kuwa nchi inayouza silaha kwa wingi zaidi katika miaka ijayo.

Urusi, Ufaransa, Ujerumani na China zimeungana na Marekani na kuwa nchi kubwa  zinazo ongoza kwa mauzo ya silaha.

Mauzo ya silaha kutoka Ujerumani ambayo inashika nafasi ya nne kwa mauzo ya nje ya silaha yalishuka kwa asilimia 14 kati ya mwaka 2008 hadi 2012 na katika kipindi cha kati ya mwaka 2013 hadi 2017.

Hata hivyo mauzo ya silaha kutoka Ujerumani kwa nchi za Mashariki ya Kati  yalipanda kwa asilimia 109 huku Ujerumani mwaka huu ikisema itazuia kuidhinisha mauzo hayo kwa yeyote anayejihusisha katika mgogoro nchini Yemen.

Mwandishi:Ashutosh Pandey

  Tafsiri    : Isaac Gamba/dw

Mhariri     : Gakuba. Daniel