Mataifa yanayoendelea yasusia majadiliano ya Copenhagen | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mataifa yanayoendelea yasusia majadiliano ya Copenhagen

Mataifa hayo yanazishutumu nchi za Magharibi kujaribu kutaka kuufutilia mbali mkataba wa Kyoto.

default

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, Yvo de Boer.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa unaoendelea mjini Copenhagen-Denmark leo umekwama baada ya mataifa yanayoendelea kususia na kuondoka katika majadiliano muhimu, huku nchi za Afrika zikizishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kutaka kuufutulia mbali mkataba uliopo sasa wa Kyoto. Mazungumzo hayo yalishindwa kuanza katika muda uliopangwa kutoka na mataifa ya Afrika kususia majadiliano hayo yaliyokuwa na lengo la kumaliza mvutano uliojitokeza katika masuala kadhaa, siku nne kabla viongozi 110 wa dunia hawajakubaliana kuuidhinisha mkataba mpya wa hali ya hewa unaotaka kudhibiti ongezeko la ujoto duniani, ambao wanasayansi wanasema huenda ukaleta zaidi hali ya ujoto kupita kiasi, mafuriko na kuongezeka kwa viwango vya bahari. Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa mataifa yanayoendelea yaliondoka katika makundi ya majadiliano mwanzoni mwa wiki ya pili ya mazungumzo hayo.

Hatua hiyo iliungwa mkono na G-77

Hatua ya kundoka katika majadiliano hayo ilianzishwa na mataifa ya Afrika, yakiungwa mkono na nchi za mataifa yanayoinukia ya G-77. Mkuu wa kundi la mataifa ya Afrika katika mkutano huo, Kamel Djemouai, amesema mataifa yaliyoendelea yanajaribu kufifisha mazungumzo hayo yanayohusisha mataifa 192. Djemouai amesema mipango ya mataifa tajiri yanamaanisha kuwa mataifa ya Afrika yatakubaliana na kutupiliwa mbali kwa chombo pekee cha halali kilichopo sasa. Mataifa hayo yanayoendelea yamekataa kuendelea na majadiliano hayo hadi hapo mazungumzo kuhusu mkataba wa Kyoto yatakapopewa kipaumbele zaidi. Mkataba wa Kyoto ambao unataka kupunguzwa matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira, unazibana nchi tajiri, lakini sio nchi masikini. Awamu ya kwanza ya ahadi zilizotolewa chini ya mkataba wa Kyoto inamalizika mwaka 2012, na mataifa ya Afrika yanataka kuwepo kwa mikakati ya mipango ya muda mrefu. Hatua ya mataifa yanayoendelea kususia majadiliano hayo ni pigo jingine kwa mkutano huo wa Copenhagen ambao tayari umegubikwa na mivutano kadhaa ukiwemo ule wa China na Marekani baada ya nchi hizo kuzozana kuhusu nani anastahili kubeba lawama kutokana na kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha, China imezishutumu nchi tajiri kwa kushindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira.

Viongozi mbalimbali wanayazungumziaje majadiliano hayo?

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na athari za mabadiliko ya hali ya hewa-UNFCCC, Yvo de Boer, anatabiri kuwa majadiliano hayo yatarejea katika hali ya kawaida muda mchache ujao. Waziri wa Mazingira wa Uingereza, Ed Miliband, ametoa wito kwa wajumbe wa majadiliano kufanya jitihada za kumaliza mkwamo unaoendelea katika mazungumzo hayo ya hali ya hewa. Awali Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd alionya kuwa mazungumzo hayo ambayo yameingia katika hali ya mvutano yako katika hatari ya kushindwa. Waziri huyo Mkuu wa Australia alisema kuna hatari kubwa kwamba kutakuwa na maoni tofauti kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea.

Mwandishi: Garce Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L220
 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L220
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com