1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Mataifa ya Ulaya yafanya kongamano kuichangia fedha Sudan

Admin.WagnerD15 Aprili 2024

Ufaransa na Ujerumani zimefanya kongamano la kimataifa la wafadhili mjini Paris ili kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu inayohitajika haraka huko Sudan.

https://p.dw.com/p/4emqy
Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Sudan mjini Paris, Ufaransa.
Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Sudan mjini Paris, Ufaransa.Picha: Christophe Ena/dpa/AP/picture alliance

Kongamano hilo limefanyika wakati mwaka mmoja umetimia tangu kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya  jeshi la serikali nchini Sudan na kundi la wanamgambo la RSF. 

Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ndio walioongoza kongamano hilo ambalo pia limejumuisha mashirika ya misaada yanayofanya kazi nchini Sudan na wawakilishi wa majirani wa Sudan.

Chanzo cha kidiplomasia cha ufaransa kimeeleza kuwa kutafuta fedha kwa ajili ya mzozo nchini Sudan kutaongeza matumaini na mkutano huo umenuwia kukusanya kiasi cha  Euro Bilioni moja.

Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa euro milioni 350, Ujerumani iliahidi euro milioni 244, Ufaransa  Euro milioni 110 na Marekani imeahidi  dola za kimarekani milioni $147.

Nchini Sudan kwenyewe mapambano bado yamechachamaa

Huko Sudan mapambano makali ya umwagaji damu yanaendelea kati ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mtawala mkuu wa Sudan, na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, anayeongoza kikosi cha wanamgambo cha RSF.

Moshi ukifuka mjini Khartoum kutokana na mapambano yanayoendelea Sudan
Kila uchao mapambano yaongezeka nchini Sudan.Picha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Vita nchini Sudan vilizuka mnamo Aprili 15 mwaka 2023 kati ya pande hizo mbili na tangu wakati huo hali inayoshuhudiwa katika taifa hilo ni mbaya huku miundo mbinu ikiwa imeharibiwa vibaya,na kusababisha kutolewa tahadhari ya kuzuka kwa baa la njaa.

Mamilioni ya Wasudan wameachwa bila makaazi ndani na nje ya taifa hilo.

Maelfu ya raia  wameuwawa japo idadi ya waliokufa,  huenda ikawa ni kubwa zaidi kuliko na inayokadiriwa. Kila upande katika vita hivyo umekuwa ukilaumiwa juu ya kufanya uhalifu wa kivita na kila upande umekuwa ukikanusha tuhuma hizo.

Mtazamo wao mkali wa kutawala Sudan umechochea janga kubwa zaidi la wakimbizi duniani, shirika la  Umoja wa Mataifa la wakimbizi linakadiria kuwa  zaidi ya watu milioni 8.6 wamekimbia makazi yao na kuelekea maeneo mengine ya Sudan  na nchi jirani huku makadirio mengine yakionesha kuwa idadi ya wakimbizi hao nia zaidi ya milioni 9.

Pande hasimu zalaumiwa kutenda uhalifu na mauaji raia wasio na hatia

Athari za mzozo wa Sudan
Mzozo wa Sudan umewalazimisha mamia kwa maelfu kuikimbia nchini hiyo.Picha: Eva-Maria Krafczyk/dpa/picture alliance

Mashambulio ya mizinga, makombora na mashambulizi ya anga yameathiri karibu kila kona ya taifa hilo la Afrika, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.

Kumekuwa na kuzorota kwa kiasi kikubwa katika hali ya kibinadamu, huku njaa ikinyemelea katika mikoa kadhaa na uhaba mkubwa wa dawa na bidhaa nyingine muhimu.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la  Amnesty International  lilisema kuwa mwaka jana lilirekodi uhalifu wa kivita uliyofanywa na pande zote mbili, ikijumuisha vifo vingi vya raia,mashambulizi ya makusudi na ya kiholela na ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana.

Mkutano wa Paris umeanza na mashauriano ya kisiasa, ambapo zaidi ya mawaziri 20 wanatarajiwa kuhudhuria, hasa kutoka Sudan, nchi jirani, pamoja na wawakilishi muhimu wa mashirika ya kimataifa.