Mataifa ya Afrika Mashariki yahofia Ebola | Masuala ya Jamii | DW | 17.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

EBOLA

Mataifa ya Afrika Mashariki yahofia Ebola

Uganda, Kenya na Tanzania, mataifa matatu waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanahofia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola ambao umeshaangamiza maisha ya watu 1,400 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Siku ya Jumapili (16 Juni) Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, alitoa onyo la tahadhari ya ugonjwa huo, baada ya watu kadhaa kugunduliwa na Ebola nchini Uganda.

"Ninataka kuwapa umma tahadhari kwamba kuna kitisho ya Ebola nchini mwetu," alisema Ummy Mwalimu kwenye ujumbe wake wa Twitter, ikiwa ni siku kadhaa kuwa wanafamilia waliokuwa wameenda matembezini nchini DRC walikufa magharibi mwa Uganda.

Waziri huyo alisema indhari hiyo ilikuwa ya lazima kutokana na maingiliano ya karibu kati ya watu wa Uganda na Tanzania "kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi."

Ingawa hatari kubwa zaidi iko kwenye mikoa ya Kagera, Mwanza na Kigoma iliyo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, lakini kwa mujibu wa waziri huyo wa afya "kutokana na kasi ya haraka kusambaa kwa ugonjwa huo, nchi nzima imo hatarini." 

Siku ya Jumamosi (Juni 15), waziri huyo alianza ziara kwenye mikoa hiyo kwa lengo la kuthathmini hatua za kuchukuliwa kwenye bandari na vituo vya mipakani ili kuzuia uwezekano wa Ebola kuingia na kusambaa. 

Hadi sasa, taifa hilo kubwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki halijawahi kukumbwa na visa vyovyote vya ugonjwa huo wa kuambukiza ambao hupelekea kutapika, homa kali na kuharisha, kufelisha mifumo ya ini na figo na wakati mwengine uvujaji damu ndani na nje ya kiwiliwili.

Wasiwasi nchini Kenya

Uganda Ebola (picture-alliance/AP Photo/IRC/B. Wise)

Indhari ya wizara ya afya nchini Uganda kuhusu ugonjwa wa Ebola katika kituo cha mpakani mwa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wilayani Kagadi.

Hayo yakijiri, siku ya Jumatatu (Juni 17) mamlaka katika Kaunti ya Kericho nchini Kenya zilisema ziko kwenye hali ya tahadhari baada ya mtu mmoja kushukiwa kuwa na Ebola.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa mwanamke mmoja aliyekuwa ametoka mji wa mpakani mwa Uganda wa Malaba kwenye Kaunti ya Bosia kumuona mwenza wake aligunduliwa kuwa na homa kali katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho.

Bado, hata hivyo, haikuwa imethibitishwa kuwa ameambukizwa kweli ugonjwa huo. Afisa wa afya kwenye hospitali ya awali alipotibiwa mgonjwa huyo alisema kuwa mwanamke huyo alilalamika maumivu ya kichwa, joto kali mwilini, kuvimba uso, kuharisha na homa. 

Ebola husambazwa kupitia kugusana na damu, majimaji ya mwili, uchafu au viungo vya mwathirika, au hata vitu vilivyogusana na majimaji hayo. 

Mripuko wa sasa nchini DRC ni mkubwa kabisa katika siku za karibuni tangu ule ulioyakumba mataifa ya Liberia, Guinea na Sierra Leone kati ya mwaka 2014 na 2016 ambao uliuwa zaidi ya watu 11,300.

WHO yatoa kauli

DR Kongo Butembo Beisetzung von Ebola-Opfern (AFP/J. Wessels)

Familia zikishuhudia wapendwa wao wakizikwa na wafanyakazi wa huduma za afya baada ya kufa kwa Ebola mjini Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tarehe 16 Mei 2019.

Hata hivyo, mnamo Ijumaa (Juni 14), Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema mripuko huo bado haujafikia kiwango cha kutangazwa kuwa "hali ya dharura kimataifa", ikimaaanisha kuwa ingelihitajia hatua za pamoja za kimataifa.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa huitangaza hali kuwa ya dharura kimataifa pale tu ugonjwa wa mripuko unapoonesha hatari ya kuvuuka mipaka ya nchi ulipoanzia.

Watu wawili kutoka familia moja nchini Uganda, mwanamke na mjukuu wake wa miaka mitano, walikufa kwa Ebola wiki moja baada ya kwenda nchini DRC kumuhudumia ndugu yao aliyekuwa mgonjwa taabani na kuhudhuria maziko.

Mdogo wa kiume wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu ameambukizwa na watu wengine kadhaa wa familia yao wamewekwa kwenye kambi ya uchunguzi na matibabu.

Hadi sasa hakuna mkasa wowote wa mgonjwa wa Ebola aliyeambukizwa akiwa ndani ya Uganda.

AFP/AP

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com