Mashirika yasiyo ya kiserikali yaipinga mikataba ya EPA | Masuala ya Jamii | DW | 23.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mashirika yasiyo ya kiserikali yaipinga mikataba ya EPA

Loius Michel akabiliwa na wabunge na watetezi wa makundi ya kijamii nchini Solvenia

Waziri wa Italia anayehusika na maswala ya Ulaya Emma Bonino, (kushoto) akizungumza na kamishna wa Ulaya anayehusika na maendeleo Louis Michel

Waziri wa Italia anayehusika na maswala ya Ulaya Emma Bonino, (kushoto) akizungumza na kamishna wa Ulaya anayehusika na maendeleo Louis Michel

Mashirika yasiyo ya kiserikali yameukosoa Umoja wa Ulaya kuhusiana na mikataba yake na nchi za Afrika, Karibik na Pacif, ACP. Watetezi wa makundi ya kijamii wanasema mikataba kati ya umoja huo na nchi hizo za ACP inayojulikana kama mikataba ya EPA, haitazinufaisha nchi hizo. Alipowasili katika mkutano wa pamoja kati ya wabunge wa Ulaya na wabunge wa nchi za Afrika, Karibik na Pacifik, ACP, mjini Ljubljana nchini Slovenia, kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maendeleo, Louis Michel, alikabiliwa na wabunge na watetezi wa makundi ya kijamii na ujumbe uliosema mikataba ya EPA iliyotayarishwa katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, haitazifaa nchi za ACP.

Louis Michel aliwaambia watetezi hao hakubaliani nao na ikiwa wanataka waendelee kubakia maskini basi waipinge mikataba hiyo ya EPA.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, Loius Michel, aliyekuwa amefadhaika, aliondoka eneo kulikofanyika maandamano hayo dhidi yake, akiwashauri waandamanaji wasome vijarida vya maelezo ya mikataba ya EPA wapate habari zaidi. Ingawa Loius Michel inasemekana anapenda kutoa ushauri wa aina hiyo wakati anapokabiliwa na maswala nyeti, Ulaya bado inazipunja nchi zinazoendelea katika maswala ya biashara na misaada.

Mikataba ya ushirikiano ya EPA inajadiliwa kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Karibik na Pacifik pasipo kuwepo mkataba wa kimataifa wa kibiashara. Mikataba hiyo imekabiliwa na utata kwa sababu nchi za ACP zinasema Umoja wa Ulaya unazitaka nchi hizo ziyafungue masoko yake ili uweze kuuza bidhaa zake huku ukiziruhusu bidhaa kidogo kutoka nchi za ACP kuingia katika nchi za umoja huo.

Makundi ya kijamii yaliyoshiriki kwenye mkutano wa pamoja wa wabunge ni pamoja na asasi isiyo ya kiserikali ya misaada na maendeleo barani Ulaya, CONCORD, jukwaa la ushirikiano wa kimaendeleo na misaada ya kiutu nchini Slovenia, SLOGA, muungano wa wakulima wa Afrika Mashariki, EAFF na jukwaa la wakulima wadogo mashariki na kusini mwa Afrika, ESAFF.

Wanachama wa mashirika ya wakulima barani Afrika pia walisafiri kwenda nchini Slovenia kupaza sauti zao zisikike. Walilikumbusha bunge kwamba zaidi ya thuluthi mbili za watu wanaokabiliwa na njaa duniani kote ni wakulima.

Elisabeth Mpofu, mwakilishi wa wakulima wa nchi za Afrika, Karibik na Pacifik, amesema mikataba ya EPA haitakiwi kuhatarisha kipato cha wakulima bali inatakiwa iwalinde waendelee kujikimu kimaisha. Bibi huyo ameongeza kusema kwa vile ilivyo hivi sasa, mikataba ya EPA inawaweka katika mashindano makali yasiyo ya haki.

Tatizo la kukosekana uwazi

Kuwepo uwazi ni swala lengine la utata katiba mikataba ya EPA. Wabunge kutoka nchi za ACP na wanachama wa makundi ya kijamii wamekasirishwa na kutokuwepo mashauriano ya kutosha. Mashauriano kuhusu mikataba ya EPA yamefanyika kwa kiwango kikubwa kwenye vikao vya faragha.

Marjan Huc wa shirika la SLOGA amesema wanataka kuona nchi za ACP zikishika usukani katika biashara na hilo linaweza kuhakishwa ikiwa wabunge na makundi ya kijamii yatashirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa kuunda mikataba ya EPA.

Ibrahim Nouhoum wa shirika la SLOGA naye amesema watu maskini wamechoka. Kuna watu wengi wanaokabiliwa na njaa katika duniani hii na kamishna wa Umoja wa Ulaya anatakiwa awasikilize watu maskini zaidi duniani.

Wazo kwamba Umoja wa Ulaya hautimizi majukumu yake kwa nchi zinazoendelea linakubalika kwa kiwango kikubwa nje ya halmashauri ya umoja huo na bado ni la msingi hata baada ya kikao kati ya wabunge wa umoja huo na wa nchi za ACP uliofanyika juma lililopita nchini Slovenia.

Marc Maes wa shirika la 11.11.11 na ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la biashara la nchi za ACP katika shirika la CONCORD barani Ulaya, amesema miaka mitano imepita tangu mashauriano kuhusu mikataba ya EPA yalipoanza, lakini kufikia sasa halmashauri ya Umoja wa Ulaya haina mambo mengi ya kuonyesha. Maes amesema Ulaya imekuwa ikiimarisha soko lake la ndani kwa miaka 50 na nchi za ACP hazitarajiwi kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitano.

Kumekuwa na shinikizo kubwa

Marc Maes anasema hii sio sababu pekee ya kuikataa mikataba ya EPA. Amesema mikataba hiyo inatakiwa pia itupiliwe mbali kwa sababu ilikamilishwa kwa haraka na chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa halmashauri ya Ulaya. Licha ya hayo, nchi 15 pekee kati ya nchi 78 za Afrika, Karibik na Pacifik, zilikuwa zimekamilisha makubaliano hayo na Umoja wa Ulaya kufikia tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana, tarehe ya mwisho iliyowekwa kusainiwa kwa mikataba ya EPA.

Miongoni mwa waliosema walishinikizwa ni Loius Straker, mbunge wa St Vincent na Grenadines katika eneo la Karibik. Aliliambia shirika la CONCORD kwamba walilazimika kusaini mikataba ya EPA kwa kuwa kama hawangefanya hivyo wangeongezewa kodi zaidi. Hawakuwa na chaguo lengine.

 • Tarehe 23.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DT2O
 • Tarehe 23.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DT2O
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com