1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Mashambulizi ya Israel yatikisa Tehran

27 Machi 2026

Mashambulizi makubwa ya Israel katikati ya Tehran yamechochea ongezeko la maafa Iran na Lebanon, huku Marekani ikiongeza shinikizo kwa Iran.

https://p.dw.com/p/5BEme
Iran Teheran 2026 |
Mapigano yameongezeka kwa kasi, na hali ya kibinaadamu Iran inazidi kuwa mbaya.Picha: Iranian Red Crescent Society/Handout/REUTERS

Jeshi la Israel limethibitisha kufanya mashambulizi makubwa katikati ya mji mkuu wa Iran, Tehran, huku miripuko mikubwa ikisikika na moshi mzito ukionekana juu ya anga la mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mashambulizi haya yanakuja vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran vikifikia kiwango cha hatari zaidi katika wiki za karibuni.

Mashambulizi ya leo yanatokea siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahirisha tishio lake la kuishambulia mitambo ya nishati ya Iran, anayoitaka ijisalimishe kwa kukubaliana na mpango wake wa kusitisha vita wenye vipengele 15.

Trump amesema ameongeza muda hadi Aprili 6 ili Iran iufunguwe tena Mlango Bahari wa Hormuz ambao ni njia hiyo muhimu ya kimkakati, akidai mazungumzo "yanaendelea vizuri,” ingawa Iran inasisitiza kuwa hakuna mazungumzo yoyote ya moja kwa moja yanayoendelea kuhusu pendekezo lake la kuvimaliza vita hivyo vilivyoanzishwa na Marekani na Israel.

Wakati huo huo, maelfu ya wanajeshi wa Israel wamevuuka mpaka na kuingia Lebanon, wakilenga kudhibiti eneo lote kusini mwa Mto Litani, takribani kilomita 30 kutoka mpaka wa Israel. Mapigano yameongezeka kwa kasi, na hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 1,900 wameuawa nchini Iran, karibu 1,100 Lebanon, na 18 Israel. Wanajeshi watatu wa Israel wameuawa Lebanon, huku wanajeshi 13 wa Marekani wakiripotiwa kupoteza maisha. Mamilioni ya watu Iran na Lebanon wanalazimika kuyahama makaazi yao.

Katika jitihada za kidiplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amezungumza kwa simu na mawaziri wenzake wa Uturuki na Pakistan, wakijaribu kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran ili kupunguza mzozo unaoendelea kupanuka.

Kwenyewe nchini Israel, shinikizo la ndani pia linaongezeka. Kundi la wazazi wa wanajeshi limemuandikia barua Mkuu wa Majeshi, likitaka kusitishwa kwa operesheni ya ardhini nchini Lebanon, wakisema wanasiasa wako tayari "kutoa kafara watoto wao.”

Hali ya kibinaadamu ni mbaya

Mashirika ya kibinadamu yanaonya kuhusu maafa makubwa, hasa nchini Iran, ambako Shirika la NRC linasema maeneo mengi ya Tehran yameharibiwa vibaya na mamilioni ya watu wako hatarini kukimbia nchi.

Iran Teheran 2026 |
Mwanamume akipokea usaidizi katika eneo la shambulio lililolenga jengo la makazi, katikati ya mzozo wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, mjini Tehran, Iran.Picha: Majid Asgaripou/WANA/REUTERS

Hali ya kibinadamu nchini Iran inazidi kuwa mbaya, huku mamlaka za Iran na mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiripoti uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema:

‘Wahudumu wa misaada ya kibinadamu nao hawako salama dhidi ya mapigano haya. Kufikia jana, Wizara ya Afya ya Iran iliripoti vifo 23 na majeruhi 112 miongoni mwa wahudumu wa afya, huku Shirika la Msalaba Mwekundu likisema kuwa kumekuwa na kifo kimoja na majeruhi 14 miongoni mwa wahudumu wa misaada hadi leo. Mapigano yamewalazimu watu kuhama na kwenda maeneo salama zaidi, jambo linaloongeza hatari zao na mara nyingi kukatiza upatikanaji wao wa mahitaji muhimu, huduma za msingi na njia za kujipatia riziki.'”

Kwa upande mwingine,Iran imezindua tena mashambulizi ya makombora kuelekea Israel, na tahadhari zimetolewa Bahrain na Qatar. Nchini Kuwait, Bandari ya Shuwaikh imeharibiwa katika shambulio, huku meli ya mizigo ya Thailand iliyoshambuliwa na Iran ikiripotiwa kukwama baada ya wahudumu wake kuikimbia.

Katika hatua nyingine, Saudi Arabia imewataka raia wake kuondoka Lebanon mara moja kutokana na kuongezeka kwa mapigano.

Wakati mvutano ukizidi kupanda, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran limewaonya raia wajiepushe na maeneo yenye wanajeshi wa Marekani, likidai Marekani na Israel wanatumia raia kama "ngao za binadamu.”