Mashambulio ya mabomu yatikisa Baghdad | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashambulio ya mabomu yatikisa Baghdad

Hali ya usalama na kisiasa nchini Iraq inazidi kusambaratika leo hii mashambulio matatu ya mabomu yameuwa takriban watu 69.

Serikali ya Iraq yaelekea kusambaratika

Serikali ya Iraq yaelekea kusambaratika

Tukianzia na hali ya usalama leo hii mashambulio ya mabomu yameua watu sio chini ya 69 katika eneo la mji wa Baghdad na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Katika shambulio baya kabisa mshambuliaji aliwasha moto katika tanki kubwa la mafuta katika kituo cha mafuta magharibi mwa mji wa Baghdad na kusababisha mripuko ambao uliua watu kiasi cha 50 na kujeruhi wengine 60 zaidi.

Kwa mujibu wa mkaazi mmoja katika eneo hilo alisikia mripuko mkubwa katika nyumba moja ambayo iliharibika vibaya na alipofikia nyumba hiyo aliona moshi ukitoka ndani ya nyumba hiyo.

Mtatibu mmoja kwenye hospitali iliyokaribu ya Yarmuk alisema kitengo cha dharura kinajitahidi kukabiliana na wimbi kubwa la watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo.Mtatibu huyo anasema majeruhi wengi wamechomeka vibaya na wamebidi kulazwa.

Mapema kabla ya shambulio hilo shambulio jingine lilitikisha eneo la bishara mjini Baghdad ambapo watu 16 waliuwawa na wengine 14 kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa Brigadia Generali Qassim Atta ambaye ni msemaji wa shughuli za usalama mjini Baghdad shambulio hilo lilitokea karibu na soko la kuuza bidhaa za elektroniki la Karradda Harij.

Shambulio hilo lilisababisha hali ya taharuki kwa wakaazi ingawa hadi sasa haijabainika ni nani aliyetega bomu hilo kwenye mtaa huo unaokaliwa na idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi wa kishia Abdel Aziz al Hakim.

Katika mji wa Dura hali pia ilikuwa ya mashaka watu watatu waliuwawa kwenye shambulio la bomu la kutegwa kando ya barabara.

Wakati hayo yakiendelea mivutano ya kisiasa nayo inazidi kujitokeza.

Mapema hii leo kundi la mawaziri sita wakisunni waliwasilisha barua zao za kujiuzulu kwenye serikali ya waziri mkuu Nuri Al Maliki inayodhibitiwa na washia.

Hata hivyo mbunge Rafie al Issawi aliyetoa tangazo la kujiuzulu kwa kundi hilo la wasunni amesema Tareq al Hashemi ataendelea kubakia kuwa makamu wa rais.

Ameongeza kusema wabunge wakisunni 44 wataendelea kuhudhuria vikao vya bunge vitakapoanza tena mnamo mwezi sepetemba.

Lakini ameonya kwamba ikiwa vyama vingine vya kisiasa havitakuwa makini katika mpango wa kisiasa watafikiria upya juu ya kujiunga na mpango huo wa kisiasa.

Tangazo hilo la kujiondoa kwa wasunni limekuja baada ya mivutano ya zaidi ya mwezi mmoja baina ya kundi hilo na serikali ya waziri mkuu AL Maliki ambayo ilikasirishwa mno na vitisho vya wasunni vya kutaka kujitenga kisiasa ikiwa madai yao hayatatekelezwa.

Kundi la Wassuni linaishutumu serikali ya al Maliki kwa kushindwa kukabiliana na wanamgambo wakishia na utesaji pamoja na kukamatwa raia wa Iraq walio wa madhehebu ya wasunni madai ambayo yamepingwa mara kadhaa na serikali..

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com