Marekani yataka uchaguzi wa amani Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 02.03.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Marekani yataka uchaguzi wa amani Kenya

Marekani imewaasa Wakenya kuchaguana kwa amani, huku wakijiandaa kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatatu ijayo, Machi 4.

U.S. President Barack Obama speaks during a news conference at the White House in Washington, January 14, 2013. REUTERS/Jonathan Ernst (UNITED STATES - Tags: POLITICS)

Barack Obama Pressekonferenz

Uchaguzi wa Jumatatu ijayo ni wa kwanza tangu ule wa mwaka 2007 ambao ulikumbwa na machafuko ya kikabila ambapo watu takriban 1,000 walipoteza maisha na wengine takriban 600,000 kulazimika kuyakimbia makazi yao.

"Huku Wakenya wakielekea uchaguzini kutumia haki yao muhimu ya msingi, tuna matumaini kwamba Wakenya wote, bila kujali jinsia, kabila, dini au eneo wanakota, watatumia haki yao ya kupiga kura kwa amani na kusaidia kuhakikisha uchaguzi wa Kenya unafanyika kwa uhuru, haki na uwazi na kuweka mbele masilahi ya pamoja ya nchi yao," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Patrick Ventrell.

Ventrell amezungumzia dola milioni 35 za msaada wa Marekani kwa ajili ya Kenya kwa lengo la kusaidia mchakato wa mageuzi ya sheria za uchaguzi na matayarisho mengine tangu mwaka 2010. Amezungumzia pia msaada wa dola milioni 90 kwa ajili ya mageuzi ya katiba na kusuluhisha mizozo tangu mwaka 2008. Fedha hizi pia zimetumika kuyasaidia mashirika ya kiraia na makundi ya vijana.

"Tuko pamoja na Wakenya wote waliojitolea kwa dhati kwa ahadi ya katiba mpya na kwa ajili ya mustakabali wa amani, maendeleo na demokrasia zaidi," amesema Ventrell.

Odinga na Uhuru waongoza kura za maoni

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga na naibu wake Uhuru Muigai Kenyatta, ndio wanaoongoza katika orodha ya wagombea wanane wa urais. Kwa pamoja, Odinga na Uhuru wametumia zaidi ya dola milioni 200 kwa ajili ya kampeni zao za kisiasa kujinadi na kuomba kura kwa Wakenya.

Kenya's Prime Minister Raila Odinga (C) waves alongside his Coalititon for Restoration of Democracy (CORD) alliance partners, his running mate Kalonzo Musyoka (L) of Wiper Democratic movement party and Moses Wetangula (R) of Ford party during a political rally in the coastal town of Malindi on February 9, 2013. Odinga, the presidential candidate for Coalition for Reforms and Democracy (CORD) and his running mate Kalonzo Musyoka campaigned in Mombasa and along Kenya's coast over the weekend in the build up to Kenya's general elections slated to be held on March 4, 2013. AFP PHOTO/ Will BOASE (Photo credit should read Will Boase/AFP/Getty Images)

Waziri mkuu, Raila Odinga

Rais Mwai Kibaki, ambaye ushindi wake dhidi ya Odinga mnamo mwaka 2007 uliibua wimbi la machafuko yaliyodumu miezi kadhaa na kuwalazimu mamia kwa maelfu ya Wakenya kuyakimbia makazi yao, amemaliza muda wake madarakani baada ya kutawala kwa awamu mbili. Analazimika sasa kujiuzulu kwa kuwa katiba haimruhusu kugombea awamu nyengine.

Marekani imesema Kenya inakabiliwa na fursa muhimu ya kihistoria katika uchaguzi wa wiki ijayo na imewataka Wakenya wote kumchagua rais wao mpya kwa amani. Wagombea wadhifa wa urais wameahidi hakutatokea tena umwagaji damu ulioshuhudiwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Lakini kuna wasiwasi mkubwa na Marekani inayafuatilia kwa karibu sana matukio nchini humo, ikisema ni wakati kwa Kenya kuchukua hatua nyengine ya kishujaa katika kuitekeleza kikamilifu katiba yake mpya na kuimarisha demokrasia yake.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE

Mhariri: Hamidou, Oummilkheir

DW inapendekeza