Marekani yatafuta masikillizano na dunia kupitia mazingira? | Masuala ya Jamii | DW | 22.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Marekani yatafuta masikillizano na dunia kupitia mazingira?

Ukiwa umedhoofishwa na hali mbaya ya kisiasa, utawala wa Rais Barack Obama unajaribu kutafuta mapatano na ulimwengu kuhusiana na suala tete la uchafuzi wa mazingira.

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Utawala wa Rais Barack Obama unajaribu kujenga hali ya kuaminiana na mataifa mengine makubwa yanayochafua hali ya hewa, badala ya kuchukua njia yenye tamaa ya kutafuta upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira katika mkutano wa dunia wa mazingira utakaofanyika huko Cancun nchini Mexico mwezi huu.

Baraza la Seneti la Marekani limeshindwa kupitisha muswada wa mazingira majira ya joto mwaka huu na Warepublican wamepata udhibiti wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi wa majimbo uliofanyika mwezi Novemba, na kuweka mbali hatua yoyote kubwa ya rais Barack Obama kupambana na hali ya kuongezeka kwa ujoto duniani hadi pengine mwaka 2013.

Hii ina maana wajumbe wa majadiliano kuhusu tabia nchi kutoka Marekani katika mazungumzo hayo , yatakayoanza Novemba 29 hadi Desemba 10 mjini Cancun, Mexico, watakosa karata turufu kuweza kuzitaka nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi kama China na India kukubaliana na utaratibu unaoshurutisha wa upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Marekani inaweza kuangalia zaidi katika kujaribu kulegeza mkwamo wake na China juu ya vipi nchi hizo zinaweza kugawana mzigo wa kiuchumi wa kupunguza utoaji wa gesi hizo kwa kushirikiana na mshirika mkubwa wa Marekani anayeinukia kiuchumi India, ili kuipa mbinyo China.

Mjumbe wa rais Obama katika masuala ya hali ya hewa Todd Stern amesema kuwa mazungumzo hayo yanapaswa kutatua malengo rahisi badala ya majukumu mazito ya kutafuta kupatikana kwa haraka muda wa mwisho kwa ajili ya mkataba mpya wa dunia ukiwa na malengo yanayoshurutisha ya upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Baadhi ya nchi zimekuwa zinataka mazungumzo hayo kuweka muda maalum, kwasababu mkataba wa Kyoto , ambao unazitaka nchi zile zilizoendelea kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi hizo, unamalizika mwaka 2012.

Badala yake, Marekani, ambayo haijajiunga na mkataba wa Kyoto, itasisitiza ahadi yake ya upunguzaji iliyotoa mwaka jana katika mkutano wa mjini Copenhagen. Obama aliahidi wakati huo kuwa Marekani, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa gesi nyingi zaidi zinazoharibu mazingira kuliko nchi nyingine yoyote, itapunguza uchafuzi wa mazingira kwa kiasi cha asilimia 17 kutoka katika kiwango cha mwaka 2005 ifikapo mwaka 2020. Na Obama hatajitoa katika lengo hilo.

Christiana Figueres , mkuu wa sekretariati ya mabadiliko ya tabia nchi ya umoja wa mataifa, amesema wiki iliyopita kuwa , dunia kwa hakika inaitarajia Marekani kutimiza ahadi yake. Wajumbe wa Marekani katika majadiliano hayo watataka kuweka msingi kwa ajili ya ushirikiano mkubwa zaidi katika kupambana na utoaji wa gesi hizo katika kiwango cha dunia, kama vile msaada kwa mataifa yanayoendelea na uwazi kuhusu upunguzaji wa gesi hizo. Lakini mbinyo unaongezeka. Iwapo hatua za maendeleo hazitafikiwa katika maeneo hayo mwaka huu mjini Cancun pamoja na mazungumzo ya mwakani nchini Afrika kusini , wengi watajiuliza iwapo mazungumzo yanayoandaliwa na umoja wa mataifa ni jukwaa sahihi la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi hususan wakati wanasayansi wanasema kuwa mwaka 2010 utakuwa na ujoto zaidi katika rekodi zao.

Na kama Obama atashindwa katika uchaguzi wa mwaka 2012, hakuna uhakika kuwa mshindi wa uchaguzi wa Marekani atachukulia hatua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa, kuwa ni jambo la kupewa kipaumbele.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mhariri: Maryam Dodo Abdallah

 • Tarehe 22.11.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QFSp
 • Tarehe 22.11.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QFSp

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com