1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Israel wajadili jinsi ya kuikabili Iran

14 Oktoba 2021

Marekani na Israel zimesema jana kwamba zinatafuta mpango mbadala wa kukabiliana na Iran iwapo haitarudi kwa nia njema kwenye mazungumzo ya kuokoa mkataba wa nyuklia wa kihistoria uliosainiwa mnamo mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/41fK7
US-Außenminister empfängt Kollegen aus Israel und den Emiraten
Picha: Andrew Harnik/AP Pool/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na wa Israel Yair Lapid hawakutoa maelezo zaidi juu hatua gani watakazoamua kuchukua iwapo Iran itagoma kushirikiana nao.

Kuna hatua kadhaa zisizo za kidiplomasia zinazoweza kuzingatiwa, ikiwa ni pamoja na kuiongezea vikwazo vya kiuchumi, au hatua za kijeshi.

Lakini kipaumbele cha serikali ya Biden kimekuwa ni kufufua makubaliano hayo ya nyuklia, na kushindwa kufanikisha hilo itakuwa pigo kubwa kwa malengo ya sera yake ya kigeni.

Israel haikuwahi kushriki makubaliano hayo ya nyuklia, kwani Waziri Mkuu wa zamani wa Benjamin Netanyahu, aliupinga mkataba huo uliosimamiwa na Barack Obama wakati wa utawala wake. Lakini baadae Donald Trump aliitoa Marekani mnamo mwaka 2018.

Soma zaidi: Waziri mkuu wa Israel Bennet aishambulia Iran

Aidha waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu pia alishiriki mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Washington.

Na viongozi hao watatu wameafikiana kupanua kile kinachojulikana kama "Makubaliano ya Abraham", yaliyosimamiwa na Trump na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu.

Mkutano huo umefanyika huku Iran ikiwa imeashiria kuwa iko tayari kurudi katika meza ya mazungumzo na Marekani mjini Vienna, lakini bila ya kutoa tarehe maalumu. Halikadhalika Iran imekuwa ikiendelea na shughuli zake za kinyuklia ambazo zilikuwa zimebanwa kulingana na maafikiano ya makubaliano hayo ya nyuklia.

Ikilazimika Israel haitasita kutumia nguvu dhidi ya Iran

"Tungependa kuona sote tukirudi kwenye makubaliano ya JCPOA. Lakini majibu ya Iran, au tuseme kukaa kwake kimya wake, kunavunja moyo. Na hivyo tunaiangalia kwa makini sana Iran. Kama alivyosema waziri wa Israeli, tuko tayari kuchukua hatua nyingine ikiwa Iran haitabadilika," ameonya Blinken.

Österreich Gebäude des Hauptsitzes der Internationalen Atomenergie-Organisation (IAEA)
Jengo la Austria la makao makuu ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA)Picha: Michael Gruber/Getty Images

Lapid kwa upande wake hakuficha msimamo wake na alikuwa muwazi zaidi. Alionya kwamba Israel iko tayari kutumia nguvu ya kijeshi ikilazimika, kuizuia Iran kutengeneza sialaha ya nyuklia.

Aliongeza kwa kudai kwamba unafika wakati mataifa yanalazimika kutumia nguvu ili kuilinda dunia isifikwe na ubaya.

Mbali na Iran, Blinken, Lapid na Abdullah Bin Zared pia walijadili namna ya kusonga mbele na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Israeli na mataifa ya Kiarabu ikiwa umetimia mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Abraham.

Soma zaidi: IAEA: Iran yazidisha urutubishaji urani hadi asilimia 60

Bin Zayed amesema anapanga kufanya ziara ya kwenda Israel, kama Lapid alivyomtembelea Abu Dhabi mwezi Juni.

Aidha Bin Zayed amesema matarajio yake ni kwamba makubaliano hayo ya Abraham yatafufua mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

Blinken alimthibitishia kwamba utawala wa Biden unaunga mkono suluhisho la mataifa mawili, kuwa ndiyo njia bora ya kuhakikisha kunapatikana amani ya muda mrefu. Kwa namna hiyo, Wayahudi wataendelee kuwa na taifa lao la kidemokrasia na Wapalestina wataweza kuwa na nchi yao wenyewe.

Vyanzo: ap,rtre