Mapigano ndani ya Msikiti Mwekundu | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 10.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mapigano ndani ya Msikiti Mwekundu

Jeshi la Pakistan lauvamia msikiti kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa na wafuasi wa itikadi kali

Wawalilia jamaa zao

Wawalilia jamaa zao

Jeshi la Pakistan limeamuru kuvamiwa “Msikiti Mwekundu” mjini Islamabad,kwa lengo la kuwakomboa “mateka” wanaoshikiliwa na wafuasi wa itikadi kali wanaoelemea upande wa Al Qaida.Zaidi ya watu 58 wameuwawa hadi sasa.

Mapigano yanapamba moto. Ripoti zinazungumzia juu ya wahanga zaidi ya 70 waliopoteza maisha yao hadi sasa.Waasi zaidi ya 50 wamesalim amri.”Ni shambulio la mwisho la kulitakasa eneo linalodhibitiwa na wanamgambo”amesema hayo msemaji wa jeshi,jenerali Waheed Arshad.

Masaa tisaa baada ya uamuzi wa kuingilia kati,jeshi la Pakistan linasema linaidhibiti thuluthi mbili ya madrasa hiyo.”Maiti zimetapakaa kila mahala” amesema bwana mmoja aliyejificha msikitini.

Wafuasi wa itikadi kali wakiongozwa na Imam Abdul Rashid Ghazi wamekimbilia katika sehemu ya chini ya jengo hilo pamoja na wakinamama na watoto,ameongeza kusema jenerali Waheed Arshad akikikiri wakati huo huo kwamba waasi wanajibisha mashambulio kwa kufyetua risasi za rashasha,mabomu ya mkono na makombora.Kuna magaidi zaidi ya wanne waliopanda juu ya mnara wa msikiti Mwekundu ili kuendeleza hujuma zao.

“Wanawatumia wakinamama na watoto kama kinga” amesema kwa upande wake waziri wa habari wa Pakistan Tariq Azim Khan kwa simu toka Islamabad na kushadidia:

“Haya ndio yale tuliyotaka kuyaepuka.Tulizungumzia yote haya pamoja na Imam.Kwa muda wa miezi minne,ndugu wawili,Imam na nduguye wameshikilia msimamo wao ule ule,walikua wakivuta wakati tuu na kuendeleza harakati zao haramu za kuwateka watu nyara.Tumefanya kila liwezekanalo kuupatia ufumbuzi wa amani mzozo,lakini kwa bahati mbaya mazungumzo yalipovunjika kwa mara nyengine tena,wanamgambo waliokua ndani wakaanzisha mapigano tuilipokua tukiondoka.”

Mizinga na risasi zimehanikiza na moshi kutanda kutoka eneo hilo.Magari ya kusafirisha wagonjwa yanaingia na kutoka katika sehemu hiyo.Habari za hivi punde zinasema jeshi limewakomboa wanawake 27 na watoto watatu.”Miongoni mwao anakutikana Ummu Hassan na binti yake amesema jenerali Waheed Arshad,akimaanisha mke wa msimamizi wa msikiti mwekundu,Abdul Aziz,aliyekamatwa jumatano iliyopita alipotaka kukimbia akivaa nguo za mwanamke.

Kwa mujibu wa viongozi wa serikali wanamgambo wasiopungua mia moja wakiongozwa na wafuasi wa Al Qaida wameuteka msikiti huo na kuwashikilia mateka wanafunzi kati ya 300 na 400 wakiwemo wanawake na watoto.

“Jeshi halitaki kufanya pupa,ili kuepukana na balaa lisilokua na maana.” Jenarali Arshad ameongeza kusema.

“Wanafunzi wamepania kupambana kufa kupona” amesema mwanaharakati mmoja kutoka ndani ya msikiti huo.

Imam Ghazi ameshasema wako tayari kufa shahid akiahidi damu yao itasababisha “mapinduzi ya kiislam nchini Pakistan.”

 • Tarehe 10.07.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2w
 • Tarehe 10.07.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2w

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com