1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said31 Julai 2008

Magazeti ya Ujerumani leo yanazungumzia juu ya Karadzic aliefikishwa mahakamani leo.

https://p.dw.com/p/Enz3
Wafuasi wa Karadzic katika maandamano.Picha: picture-alliance/ dpa

Katika maoni yao leo, wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanasema kufunguliwa mashtaka kwa Karadzic ni mafanikio makubwa kwa jumuiya ya kimataifa.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya matatizo yanayowakabili waandishi habari nchini China siku chache tu kabla ya michezo ya olimpiki kuanza.

Kuhusu Karadzic aliefikishwa mbele ya mahakama leo gazeti la Kölnische Rundschau linasema leo siyo siku ya madikteta. Mhariri wa gazeti hilo anasema kufikishwa mbele ya mahakama kwa Karadzic ni mafanikio makubwa kwa mahakama ya Umoja wa mataifa. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba mtuhumiwa huyo wa mauaji amefikishwa mbele ya mikono ya sheria baada ya miaka 13 ya kujificha.Lakini anakumbusha kwamba katika mambo ya sheria, ni lazima kuthibitisha kwamba mtuhumiwa ana makosa- jambo ambalo siyo rahisi. Mhariri huyo anakumbusha juu ya yaliyotokea katika Ujerumani mashariki baada ya ukomunisti kusambaratika.

Gazeti la Thüringer Allgemeine pia linazungumzia juu ya Karadzic kwa kuwapongeza waliowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa mauaji.

Gazeti hilo linasema, baada ya miaka mingi ya kukutaa kushirikiana na mahakama ya kimataifa waserbia waliamua kubadili mtazamo.Mhariri wa gazeti la Thüringer Allgemeine anaeleza kuwa itakuwa vizuri kwa wananchi na serikali ya Serbia kushikilia msimamo huo, na anakumbusha kwamba bado wapo wahalifu wengine nchini.


Mhariri wa gazeti la Nordwest-Zeitung anasema viongozi wa China wanazidi kuwa na wasiwasi kadri michezo ya olimpiki inavyokaribia.

Wasiwasi huo unadhihirika katika njama za kujaribu kubana uhuru wa vyombo vya habari.Lakini mhariri anasema katika enzi hizi za kompyuta habari zinaweza kupatikana kila mahala na wakati wote.

Gazeti linaloitwa 20 Cent linazungumzia juu ya chama kinachotawala nchini Uturuki- AKP .

Chama hicho kimenusurika kupigwa marufuku na mahakama ya katiba.

Chama hicho kilikabiliwa na madai ya kutaka kuleta sheria za kiislamu nchini Uturuki. Juu ya hayo gazeti la 20 cents linakumbusha kwamba vyama vingine vya kisiasa barani Ulaya pia vina nasaba za dini.

Mfano ni chama cha CSU kilichomo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba chama hicho kinasisitiza juu ya kuwepo msalaba katika kila darasa- Jee chama hicho nacho kipigwe marufuku? Gazeti linasema hapana. Chama cha CSU cha Ujerumani na cha AKP cha Uturuki lazima viwe na jukwaa la pamoja kwa manufaa ya bara la Ulaya.