1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

29 Mei 2007

Katika maoni yao ,wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya misimamo tofauti kuhusu ulinzi wa mazingira na hali ya hewa kabla ya mkutano wa nchi nane tajiri duniani.

https://p.dw.com/p/CHSr

Waharriri hao pia wanatoa maoni yao juu ya mazungumzo ya ana kwa ana yaliyofanyika mjini Baghdad baina ya Iran na Marekani kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27.

Juu ya misimamo tofauti kuhusu ulinzi wa hali ya hewa gazeti la Die MÄRKISCHE ALLGEMEINE linasema yaelekea itakuwa vigumu kufikia mapatano na utawala wa rais Bush katika suala hilo.Mapatano hayo yanahusu kupunguza utoaji wa gesi chafu ili kupunguza ongezeko la joto duniani.

Mhariri wa gazeti hilo kutoka mji wa Potsdam anasema katika maoni yake kuwa kwenye mkutano wa nchi nane tajiri duniani itakuwa bora kuwataja wale wanaozuia kufikiwa mapatano, badala ya kufikia usikizano ambao baadae hautaleta manufaa kwa yeyote.

Mhariri wa gazeti la WETZLARER NEUE ZEITUNG pia anazungumzia juu ya suala hilo katika maoni yake na anatumia kauli bayana kabisa juu ya msimamo wa Marekani.

Anakumbusha kuwa siku chache tu kabla ya kuanza mkutano wa nchi nane tajiri duniani hapa Ujerumani, utawala wa rais Bush umefafanua msimamo wake juu ya suala la ulinzi wa mazingira. Mhariri huyo anaeleza kuwa msimamo wa bwana Bush unajibaidisha na juhudi za kulinda hali ya hewa.

Gazeti linasema msimamo huo unamaanisha kuchafua mazingira mara mbili , kwanza unachafua mazingira ya dunia nzima, na pili unavuruga mazingira ya mkutano wa viongozi wa nchi nane tajiri utakaofanyika Heiligendamm kwenye pwani ya Baltik hapa nchini Ujerumani.

Lakini gazeti la WISBADENER KURIER linampongeza Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa kuwa na moyo shadidi katika mazungumzo juu ya ulinzi wa mazingira.Gazeti hilo anasema kuwa msimamo huo unaweza kuzaa matunda kwani bila ya kuzungumza na kuishinikiza Marekani haitawezekana kusonga mbele katika suala hilo.

Mhariri anasema msimamo wa Kansela Merkel ni muhimu siyo tu kwa sababu Marekani ndiyo inayobeba lawama kubwa katika utoaji wa gesi chafu bali pia pana nchi zingine kama China na India ambazo pia zimo katika orodha ya wahalifu wa mazingira.Kinachotakiwa ni kigezo kitakachofuatwa na wote ili kuweza kufikia mwafaka.

Mhariri anasema ikiwa mkutano wa viongozi wa nchi nane tajiri utashindwa kufikia mapatano juu ya suala la mazingira , hakika hiyo itakuwa ishara ya kuvunja nguvu.

Juu ya mkutano wa ngazi ya juu baina ya Marekani na Iran ambao umefanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27, mhariri wa gazeti la ABENDBLATT anasema kuwa mazungumzo hayo hayakuwa msingi wa kujenga hali ya kuaminiana baina ya Iran na Marekani hata kama yamefanyika katika ngazi ya kibalozi. Mhariri anasema hatua ya dhati ya kukaribiana baina ya pande mbili hizo itafikiwa ikiwa sera za ikulu ya Marekani zitabadilika na ikiwa nchini Iran rais Ahmadinejad ataondoshwa pamoja na msimamo wake wa kukana maangamizi ya wayahudi.

Lakini mhariri wa gazeti la TAGESSPIEGEL anasema kufanya mazungumzo ni jambo zuri wakati wote.

Hatahivyo anakumbusha kuwa siku chache tu kabla ya mazungumzo hayo Marekani ilionesha misuli ya kijeshi kwenye Ghuba .Ilifanya mazeozi makubwa ya kijeshi ambapo askari alfu 17 walishiriki.Lakini Iran inatambua kwamba Marekani haiwezi kuzima uasi nchini Iraq bila ya msaada wake.

Naye mhariria wa gazeti la DIE WELT anaeleza kuwa mazungumzo ya jana yanaashiria mwisho wa uzito wa wahafidhina mamboleo katika Washington.